Bil 1.8/- zatumika miradi ya CSR Geita

KAMPUNI ya Mgodi wa Bucreef imetumia sh bilioni 1.8 kutekeleza miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) wilayani Geita ndani ya miaka minne kati ya mwaka 2020/21-2024/25.

Aidha Mgodi wa Bucreef umefanikiwa kuongeza kiwango cha CSR kutoka wastani wa sh milioni 450 kila mwaka hadi kufikia wastani wa sh milioni 600 kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Meneja Mkuu wa Bucreef, Isaac Bisansaba amesema hayo katika hafla ya kusaini mkataba mpya wa miradi ya CSR kwa mwaka huu wa fedha na halmashauri ya wilaya ya Geita.

SOMA: Mil 980/-kujenga maabara ya uchunguzi madini Geita

Bisansaba amesema mafanikio hayo ni matokeo ya ongezeko la uzalishaji uliofikia tani laki tano kwa mwezi kati yake tani 50,000 za madini ya dhahabu zinachakatwa na kuzlishwa kwa mwaka.

Amesema hatua hiyo imefanikisha kutoa wastani wa ajira 700 kwa mwezi na kuchangia kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja hususani kwa jamii inayozunguka eneo la mgodi wa Bucreef.

Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa kimadini Geita, Samwel Shoo amesema mgodi wa Bucreef umeonyesha ukuaji mkubwa katika matumizi ya teknolojia sahihi kiasi cha kuongeza uzalishaji.

“Suala la CSR ni utekelezaji wa sheria ya madini sura namba 123 inaelekeza kwamba kila mwekezaji ana wajibu wa kurejesha katika jamii kile anachokizalisha”, amesema Shoo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Geita, Jumanne Misungwi amesisitiza Baraza la Madiwani kuhakikisha linatoa ushirikiano wa usimamizi wa miradi ya CSR chini ya Bucreef.

Mkuu wa wilaya ya Geita, Hasheem Komba amesema kwa kutambua umuhimu wa wawekezaji ofisi yake imejizatiti kutatua changamoto zinazokwamisha uwekezaji ili kutoa fursa za kiuchumi.

Naye Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema Bucreef ni miongoni mwa migodi ya mfano katika utekelezaji wa sheria ya CSR hali inayounga mkono utekelezaji wa dira ya maendeleo.

Amesema Bucreef kwa sasa inazalisha wastani wa kilo 60 za dhahabu kwa mwezi sawa na wastani wa kilo 720 kwa mwaka hali inayodhihirisha matokeo chanya ya sera rafiki za uwekezaji nchini.

Mkazi wa kata ya Busanda, Selemani Gamala amesema Bucreef kupitia CSR imefanikisha kuboresha mazingira ya huduma za afya kupitia ujenzi wa zahanati pamoja na vituo vya afya.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kaseme, Andrea Kalamula amekiri kuwa CSR kutoka mgodi wa Bucreef imechangia kuboresha ubora wa miundombinu ya elimu kwenye maeneo yao

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button