Aagiza kuvunjwa mkataba na mkandarasi ‘tapeli’

NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Elimu, Reuben Kwagilwa ameagiza kuvunjwa mara moja mkataba wa Bogeta Engineering Ltd baada ya kubainika kughushi kipengele cha malipo ya awali katika mradi wa ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa Shule ya Sekondari Jenista Mhagama mkoani Ruvuma.
Agizo hilo limetolewa wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi huo unaojumuisha mabweni mawili, vyumba sita vya madarasa na matundu 10 ya vyoo. “Sijaridhishwa na kasi ndogo ya utekelezaji, licha ya mkandarasi kulipwa zaidi ya Shilingi milioni 80, huku kazi ikiwa bado kwenye hatua ya ujenzi wa jamvi,” alisema.
Ameongeza: “Vunjeni mkataba, fuateni taratibu za kumpata mkandarasi mwenye uwezo ili wanafunzi wapate huduma kama alivyoelekeza Rais Samia Suluhu Hassan”. SOMA: Waziri Tamisemi asifu utendaji wa Rais Samia
Mradi huo wa Sh milioni 417 unaofadhiliwa na Barrick Tanzania ulianza Mei 17, 2025 na ulipaswa kukamilika Oktoba 27, 2025 lakini hadi sasa ujenzi umesimama, hali iliyochochea hatua kali za serikali kulinda fedha za umma na haki ya wanafunzi kupata elimu bora.



