ACT wataka kiswahili iwe lugha ya kufundishia

DAR ES SALAAM; CHAMA cha ACT Wazalendo kimeishauri serikali kubadili sera na kukifanya kiswahili kuwa lugha ya kufundishia na kujifunzia kwa ngazi zote za elimu, kisha kingereza na lugha zingine zifundishwe kama masomo.

Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa chama hicho, Hamidu Bobali kupitia taarifa yake kwa umma amesema mchakato wa kutafsiri na kutunga vitabu kwa lugha ya kiswahili uanze, ili kuwezesha uwepo wa rejea za kutosha za lugha hiyo.

Bobali amesema ni vyema Tanzania kutumia Kiswahili kama lugha rasmi ya kujifunzia na kufundishia mpaka chuo kikuu, ili kurahisisha usafirishaji wa taarifa, maarifa na ujuzi kwa urahisi.

Soma pia:https://habarileo.co.tz/kasi-yazidi-kiswahili-kitumike-eac-un/

“Maendeleo ya teknolojia yameondoa kabisa vikwazo vya mawasiliano na kwa sasa biashara yoyote inaweza kufanyika bila utegemezi wa lugha fulani,” amesema Bobali.

Amesema lugha ni nyenzo muhimu katika mchakato wa kujifunza kwa maana huchochea udadisi, uvumbuzi na utatuzi wa haraka wa masuala mbalimbali.

“Tafiti zinaonesha kuwa mtoto anaelewa zaidi akifundishwa kwa lugha yake kuliko lugha ya kigeni. Watoto wanashindwa kujibu maswali na kufeli kutokana na kushindwa lugha,” amesema Bobali.

Habari Zifananazo

Back to top button