ACT Wazalendo yaahidi serikali jumuishi Z’bar, mshahara mil 1/-

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema wananchi wakimchagua ataunda serikali jumuishi.

Othman amesema hayo katika mkutano wa kampeni katika viwanja vya Kibanda Maiti Unguja.

Alisema mfumo wa serikali jumuishi kwa vyama vya siasa unatoa nafasi ya wananchi kushiriki katika ujenzi wa taifa na hivyo kuharakisha maendeleo ya wananchi.

SOMA: ACT Wazalendo wajitosa uchaguzi mkuu

‘’Nikipata ridhaa ya kuchaguliwa kuongoza Zanzibar nitahakikisha naunda serikali jumuishi itakayovishirikisha vyama vyote vya siasa katika kuiendesha kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya pamoja,’’ amesema Othman.

Amesema anakusudia kuimarisha maslahi ya watumishi wote na kwamba kima cha chini cha mshahara kitakuwa Sh milioni moja.

Othman amesema kima cha mshahara kilichopo ni kidogo na hakimuwezeshi mfanyakazi kutekeleza majukumu yake kwa ari na moyo thabiti.

‘’Nikipata ridhaa ya kuongoza nchi nitahakikisha napandisha kiwango cha mishahara kwa watumishi wa serikali ambapo kima cha chini kitakuwa Sh milioni moja ili kuongeza ari na kuweza kumudu hali ya maisha,’’ amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu amewaomba wananchi kumchagua mgombea urais wa chama hicho kwa kuwa ana uzoefu mkubwa ikiwa ni pamoja na kufahamu sheria mbalimbali na upungufu wake.

‘’Tunazo sheria nyingi zimepitwa na wakati ambazo zinahitaji marekebisho yake kwa ajili ya kuweka mustakabali mzuri wa maisha ya wananchi ambapo mwenzetu huyu Othman ni mtaalamu katika eneo hilo, kazi hiyo ataifanya,’’ amesema Jussa.

Mwenyekiti mstaafu wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji amesema matarajio yake makubwa ni kuona Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unakuwa huru na haki.

Ameeleza kufurahishwa na maandalizi ya tume hiyo katika hatua mbalimbali.

“Matarajio yangu makubwa ni kuona uchaguzi mkuu wa mwaka huu unakuwa huru na haki kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) katika hatua tofauti,” amesema Duni.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button