DAR-ES-SALAAM: CHAMA cha ACT Wazalendo kimeanza awamu ya kwanza ya kampeni ya kusajili wanachama milioni 10 katika kipindi cha miezi 10 kuanzia sasa mwezi huu.
Taarifa ya Naibu Katibu wa Habari, Uenezi, Mahusiano na Umma ACT Wazalendo, Shangwe Ayo imeeleza kuwa katika awamu hiyo itakayokamilika Aprili mwakani chama hicho kimepanga kufikia mikoa 22 yenye majimbo 225 kati ya majimbo yote 214 ya Tanzania Bara.
Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu akiwa Jimbo la Mvumi mkoani Dodoma, alisema wanaendesha kampeni ya kusajili wanachama katika mfumo wa kisasa wa ACT kiganjani kwa sababu wamedhamiria kushiriki na kushinda chaguzi ili kuongoza Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji na kushika dola mwakani.
Semu amesema Septemba mwaka huu chama hicho kitafanya awamu ya pili ya kampeni ambayo itamalizia majimbo 89 yaliyobaki ili kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa ACT Wazalendo iwe imefikia majimbo yote 2014 ya Tanzania Bara.
“Wanachama wa chama cha siasa ndio mtaji wa kwanza wa chama. Wanachama wetu pamoja na Watanzania wengine wakitupigia kura tutaongoza serikali za vijiji, mitaa na vitongoji kwa kuonesha namna bora ya kuendesha vijiji vyetu, mitaa na vitongoji vyetu kwa maslahi ya wananchi wote,” alisema. Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Isihaka Mchinjita.