ACT Wazalendo yaitaja INEC uchaguzi mitaa

DAR ES SALAAM; CHAMA cha ACT Wazalendo kimeishauri Serikali kupeleka muswada bungeni wa kutunga sheria itayosimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa chini ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).

Hatua hiyo imekuja baada ya chama hicho kudai kuwa kauli ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Dk Ramadhan Kailima kuwa ni halali kwa wizara yenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024.

Katika taarifa yake kwa wanahabari, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema chama hicho kinapinga kauli hiyo ya Dk Kailima kwa sababu haiko kisheria.

Dk Kailima alitoa kauli hiyo Juni 13, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu uboreshwaji wa daftari la wapigakura unaotarajiwa kufanyika kuanzia Julai 2024.

Ado amesema msimamo wa ACT Wazalendo ni kuwa kutotungwa kwa sheria ya kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa hakuipi nafasi TAMISEMI kusimamia uchaguzi huo kwa sababu Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa iliyokuwa inaipa madaraka TAMISEMI kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa imefutwa na kifungu cha 167 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024.

“Tunarejea rai yetu kuwa kitendo cha TAMISEMI kujitwika wajibu wa kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa kinyume na sheria za nchi ni batili na unatia doa kubwa kwa falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Ado.

Habari Zifananazo

Back to top button