AFA Fashion Night kufanyika Novemba 29

MSIMU wa pili wa Tamasha la Mitindo na Mavazi ‘AFA Fashion Night’ unatarajiwa kufanyika Dar es Salaam Novemba 29 mwaka huu na kushirikisha wabunifu na wanamitindo 500 kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Akizindua tamasha hilo Dar es Salaam juzi mgeni maalumu Haji Manara aliomba wadau kuwaunga mkono waandaaji Anna Collection ili kusaidia kupatikana kwa ajira.

Alisema wanawake wengi siku hizi wanajiingiza katika ubunifu wa mitindo na mavazi kwasababu ndiko dunia inakoelekea.

“Tukio hili limebeba taswira ya ubunifu wa mitindo na mavazi, linatoa nafasi kwa wadogo zetu, wasichana wa kitanzania, watoto wetu kuonesha kile walichonacho,”alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Anna Collections Anna Lunguya alisema kupitia Chuo chao cha ubunifu na mavazi wamefanikiwa kutoa wabunifu 500 wakiwa ndio kwanza wana mwaka mmoja.

“Tuna wanafunzi wengi wa kutoka hapa ndani ya nchi, na baadhi wanatoka Jamhuri ya Kidemokaria ya Congo (DRC), Sudan Kusini, Zambia, Kenya na Uganda hivyo, tunategemea kupata wabunifu kutoka mataifa hayo watakuja kwenye tamasha,”alisema.

Alisema tamasha hilo litaibua vijana na wanawake kuweza kuonekana na kupelekea kukuza sanaa ya ubunifu wa mitindo Tanzania.

Habari Zifananazo

Back to top button