Afrika Kusini yatangaza mgao wa umeme

SHIRIKA la Taifa la Umeme la Eskom nchini Afrika Kusini limetangaza kuanzishwa kwa mgao wa umeme, kufuatia tatizo la kukatika ghafla kwa umeme katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Tangazo hilo la mgao wa umeme limekuja kwa mshangao, hasa baada ya taarifa ya kutia moyo kutoka kwa Eskom, ambapo walieleza matumaini ya kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme ambalo limeendelea kwa miaka mingi na wakati mwingine kuathiri huduma kwa hadi masaa 12 kwa siku. Eskom ilikuwa na matumaini ya kutatua changamoto hii hivi karibuni.

Hata hivyo, katika taarifa iliyotolewa, Eskom ilieleza kuwa inawalazimu kufanya mgao wa umeme kwa kipindi kisichojulikana.

Hii ni kutokana na hitilafu nyingi zinazojitokeza katika mitambo yake mitatu ya nishati ya makaa ya mawe, ambayo ndiyo inayotumika kuzalisha umeme kwa wingi nchini humo.

Eskom, ambayo pia inakabiliwa na deni kubwa, ilieleza kuwa hatua hii ni muhimu ili kuhakikisha usambazaji wa umeme unakuwa salama, ingawa inazidi kufanya juhudi za kurekebisha mitambo ili kuondokana na tatizo hili la kukatika kwa umeme.

Chanzo: DW

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button