Afrika yashauriwa umoja kukabili athari vita Ukraine

WACHAMBUZI wa masuala ya demokrasia na uchumi wameshauri Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki zishikamane kuimarisha uchumi kutokana na vita ya Ukraine na Urusi kuzidi kupamba moto.

Rai hiyo ya wachambuzi imekuja siku chache baada ya Rais wa Marekani, Joe Biden kuipa Ukraine mabomu yenye mtawanyiko mkubwa (cluster) kupambana na Urusi.

Mabomu hayo hutawanya idadi kubwa ya mabomu madogo kutoka kwenye roketi, kombora au makombora ambayo hutawanywa angani kwenye eneo pana.

Hurushwa na kulipuka ingawa kwa sehemu kubwa hayalipuki hasa yanapotua kwenye ardhi laini au yenye unyevu.

Mhadhiri kutoka Chuo cha Diplomasia, Goodluck Ng’ingo, alisema sasa ni wakati wa nchi za Afrika  Mashariki na Afrika kwa ujumla, kushikamana kuzuia mdororo wa uchumi.

“Mdororo wa uchumi utakuwepo kama ilivyokuwa mwanzo…  tupambane na gesi asilia kupunguza makali ya uchumi,” alishauri Ng’ingo.

Kwa upande wake, mchumi kutoka Chuo cha Diplomasia, Profesa Watengere Kitojo alisema kinachofanywa na Marekani ni kuchochea vita kwa kutoa silaha kubwa kutokana na uadui wake na Urusi.

“Wanafanya hali ya kiuchumi duniani kuwa mbaya kama mwanzo, hakuna dalili ya vita hii kwisha,” alisema na kueleza umuhimu wa Tanzania kujitegemea kwenye masuala ya ngano na mbolea.

“Tuzalishe ndani ya nchi na Jumuia ya Afrika Mashariki ili kwenye vita kama hiyo, tujibebe wenyewe… tujitegemee kwenye vitu kama chakula, tumejifunza kwenye Covid 19 na vita hiyo ya Ukraine tangu ianze naamini tunaweza,” alisema.

Profesa Abel Kinyondo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema vita inayoendelea ni ya kiuchumi ikihusisha nchi za Magharibi na Mashariki.

“… mafahari wawili wakigombana nyasi ndio zinaumia, bidhaa ya mafuta, gesi itakuwa ngumu kupatikana bei itakuwa juu, mfumuko wa bei utaendelea na itakuwa ngumu kulima… tutarudi kulekule tulipotoka kwenye shida ya nishati.”

Profesa Kinyondo alishauri Umoja wa Mataifa (UN) kufanya kazi yake kuhakikisha vita inakoma.

“Tanzania tumejaaliwa tunayo mafuta pia gesi, lakini pia tunayo nishati ya jotoardhi, kama nchi tujue hatuwezi kuwa tegemezi kwenye bidhaa mtambuka kama hizo twendeni na mikakati ya kujitegemea wenyewe,” alisema.

Profesa Kinyondo alisema wakati umefika wa kuwa na vituo vingi vya gesi ili itumike kwenye magari na kwenye matumizi mengine ya nyumbani.

“Mafuta ya kupikia tuwe na mikakati tutumie vizuri alizeti, karanga, mawese tutengeneze mafuta wenyewe, ngano tuna sehemu za baridi tunaweza kulima kwa ufanisi mkubwa tu ni suala la mkakati tunatakiwa tusambaze sio tuagize,” alisema.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
3
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x