Afya ya udongo iwe kipaumbele kwa maendeleo endelevu

Shirika la kimataifa linaloshughulikia uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu (IUCN) kwa kushirikiana na Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), serikali na wadau wamesaini makubaliano ya kushirikiana katika kulinda na kuboresha afya ya udongo, kwa kuzingatia umuhimu wake katika maendeleo endelevu.
Makubaliano hayo, yanalenga kuimarisha usimamizi wa ardhi na kilimo endelevu, na kuhakikisha kuwa hatua zinachukuliwa ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na upungufu wa rutuba ya udongo ambazo zinakumba maeneo mbalimbali nchini.
Katika warsha yao ya siku mbili iliyojadili dhana ya afya ya udongo na matumizi endelevu ya ardhi, Mwakilishi wa IUCN, Antony Muhagama alisisitiza umuhimu wa mikakati ya pamoja ili kupunguza uharibifu wa ardhi, kutunza vyanzo vya maji, na kuimarisha tija katika kilimo.

Alisema makubaliano haya ni hatua muhimu kuelekea malengo ya maendeleo endelevu, ambapo kila mdau atachukua jukumu la kuhakikisha kuwa ardhi na udongo vinaendelea kuwa na afya nzuri kwa manufaa ya jamii na vizazi vijavyo.
“Afya ya udongo ni msingi wa kilimo chenye tija na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Hata hivyo, Tanzania inakabiliwa na changamoto za kupungua kwa rutuba ya udongo na uharibifu wa ardhi, changamoto zinazochangiwa na ukataji miti, matumizi mabaya ya viuatilifu, na athari za mabadiliko ya tabianchi,” alisema.
Adamu Mtaturu kutoka taasisi ya kilimo SAGCOT Centre Ltd alisisitiza umuhimu wa elimu kwa wakulima kuhusu afya ya udongo.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa tafiti zinawafikia wakulima kwa njia rahisi badala ya kubaki kwenye machapisho,” alisema.

Alihimiza pia serikali kwa kushirikiana na wadau kuboresha miundombinu ya umwagiliaji ili kukabiliana na athari za ukame unaotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Godwin Makole, alizungumzia changamoto ya upungufu wa rutuba na tatizo la tindikali katika udongo, akisema serikali inatoa msaada kwa halmashauri kwa kutoa vifaa vya kupimia udongo.
Hata hivyo, alikiri uchache wa vifaa ni jambo linalokwamisha jitihada za upimaji kulingana na mahitaji katika kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo na kufanikisha mipango ya kulinda afya ya udongo.

Mhandisi Makole alisema serikali ilitoa kwa kila halmashauri kifaa cha kupimia afya ya udongo, na mpango wake katika kukabiliana na mahitaji makubwa ni kutoa kifaa hicho kwa kila kata.
Awali Mkulima kutoka kata ya Magulilwa wilayani Iringa, Oroda Msuva alielezea changamoto za wakulima kuhusu upimaji wa udongo.
“Tunashauriwa kupima udongo lakini vifaa vya kupimia havitoshi kuhudumia wakulima wote. Serikali inapaswa kuongeza vifaa hivi ili kufanikisha kilimo cha tija,” alisema.
Naye Mdhibiti wa Visumbufu vya Mimea na Msimamizi wa Viwatifilifu kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viwatilitifu vya Mimea (TPHPA), Ramadhani Kilewa alizungumzia upungufu wa virutubisho kama fosforasi, nitrojeni, na potasiamu katika ardhi na jinsi unavyoathiri afya ya udongo.
“Matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu yameongeza changamoto hii, na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazorotesha zaidi afya ya udongo,” aliongeza.

Moses Numbi kutoka Dodoma Cement alisisitiza umuhimu wa matumizi ya chokaa ya kilimo kudhibiti tindikali ya udongo, akionyesha uwezo wa kiwanda chao kuzalisha zaidi ya tani 20,000 za chokaa kwa mwaka, ingawa uzalishaji huo umekuwa ukiathiriwa na mahitaji.
“Tuna uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 20,000 za chokaa, lakini kwa kuwa mwamko wa matumizi yake ni mdogo miongoni mwa wakulima tumekuwa tukizalisha kati ya tani 3,000 na 5,000 tu kwa mwaka,” alisema huku akihimiza umuhimu wa elimu kuhusu chokaa hiyo kuendelea kutolewa kwa wakulima.
Washiriki walikubaliana kuwa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, na wadau utahakikisha utekelezaji wa mikakati ya kulinda afya ya udongo, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, kuhamasisha matumizi ya chokaa, na kuanzisha kampeni za upandaji miti ili kulinda na kudumisha afya ya udongo kwa manufaa ya jamii na vizazi vijavyo.



