Agusta kuiwakilisha Tanzania katika onesho la mitindo Nigeria

MBUNIFU wa mavazi na mwanamitindo, Agusta Masaki, anatarajiwa kuiwakilisha Tanzania katika onesho kubwa la mitindo Africana Royal Elegance Collection litakalofanyika nchini Nigeria kuanzia Novemba 28 hadi 30, 2025.
Akizungumza na HabariLEO, Agusta amesema kuwa fursa hiyo ni hatua muhimu katika safari yake ya ubunifu na ni heshima kubwa kuiwakilisha Tanzania kwenye jukwaa la kimataifa. “Kuanzia Dar es Salaam hadi Lagos, ninaenzi nguvu, uzuri na kujiamini kwa wanawake kote duniani,” alisema Agusta.
Mbunifu huyo amebainisha kuwa miongoni mwa mavazi atakayoyawasilisha ni yale ya asili yaliyotengenezwa kwa kutumia khanga za Kitanzania kutoka Kiwanda cha NIDA pamoja na vitenge, akilenga kuonyesha utamaduni wa Tanzania kupitia mitindo ya kisasa na ya kipekee.
Agusta ameishukuru Wear Nigeria kwa nafasi hiyo adhimu, huku akiwapongeza viongozi wa serikali kwa kuunda mazingira yenye kuhamasisha wasanii na wabunifu. “Asante Wear Nigeria kwa fursa hii ya kipekee! Shukrani zangu kwa serikali yangu ya Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Wizara, BASATA na NIDA kwa kunisapoti,” alisema.
Aidha, Agusta ametoa wito kwa vijana kuendelea kutumia vipaji vyao kujiajiri na kuitangaza Tanzania kupitia sanaa mbalimbali zikiwemo mitindo, muziki na maigizo, akisisitiza kuwa sanaa ni nyenzo muhimu ya kuitangaza nchi kimataifa. SOMA: Millen Magese jaji mkuu Tamasha la Mavazi Samia



