Ajali ya Happy Nation yaua Hakimu Bukoba

 POLISI mkoani Kagera inamshikilia dereva wa Basi la Happy Nation, Shaaban Khatibu 38 mkazi wa Dare es Salaam akidaiwa kusababisha vifo vya watu wawili.

Tukio hilo inadaiwa lilitokea Barabara ya Biharamulo, Kata Ijuganyondo, Manispaa ya Bukoba, Jumanne Desemba 6, mwaka huu majira ya saa 5.30 asubuhi.-

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, William Mwampaghale amewataja marehemu hao kuwa ni Geofrey John (42),  mfanyabiashara  na Tumaini Jofrey (41), ambaye ni hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kata ya Maruku.

Amesema Geofrey na Tumaini walikuwa wamebebana kwenye pikipiki, yenye namba za usajili T308CLH, ambapo walisukumwa na mwendesha pikipiki aliyekuwa  amebeba magunia ya mkaa na kisha kuangukia uvunguni mwa gari la kampuni ya Happy Nation, yenye namba za usajili T70DFV, aina ya Youtong,  inayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Bukoba.-

Amesema polisi inaendelea kumtafuta dereva wa pikipiki iliyokuwa imebeba mkaa na kwamba uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.

Katika mitandao mbalimbali ya Whatsapp ya mjini Bukoba, kulisambazwa ujumbe wa Tanzia ulioonesha umetoka  Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kwamba na ukieleza kifo cha hakimu huyo pamoja na mumewe kwa ajali ya gari, ingawa polisi haikusema kama ni mke na mume.

‘Tanzia: Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, inasikitika kutangaza kifo cha Tumaini John Kiyeyeu-C/No.11510783 Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kolekero, Bukoba na mme wake kilichotokea mchana huu kwa ajali ya gari na kupelekea wote kupoteza maisha.

Tutaendelea kutoa taarifa kuhusiana na taratibu za mazishi,” unasomeka sehemu ya ujumbe huo.

Habari Zifananazo

Back to top button