Ajali za barabarani zifike mwisho

Baadhi ya matukio ya ajali

AJALI za barabarani zimekuwa tishio nchini.

Mbali na uharibifu mkubwa wa mali, zimegharimu maisha ya mamia ya Watanzania ambao ni nguvukazi iliyotegemewa kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Tishio la ajali hizo linaweza kudhihirika kutokana na taarifa za mfululizo wa ajali mfano tu zilizotokea mwezi huu wa Desemba.

Advertisement

Achilia mbali ajali zilizotokea miezi ya nyuma, lakini mwezi huu tangu umeanza hakuna wiki inapita bila ajali ambazo kila siku zinapoteza Maisha ya Watanzania wakubwa kwa wadogo, masikini na matajiri, wazee na vijana ni hali inayoogopesha hata mtu anapofikiria kuingia barabarani au kusafiri.

Katika kipindi cha muda mfupi tu mwezi huu imetokea ajali Biharamulo ikapoteza Maisha ya watu 11, Tanga ikapotea uhai wa watu wanane na ajali nyingine ya Morogoro wakapoteza maisha ya watu 15 na bado kuna ajali zilizohusisha magari ya watu binafsi na kupoteza maisha ya wanafamilia, orodha ni ndefu na inasikitisha.

Mfululizo wa matukio haya, yanamsukuma Rais Samia Suluhu Hassan kusema neno katika ukurasa wake wa lnstagram, aliandika, “mbali na wito wangu kwa umma na maelekezo niliyolipa Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama Desemba 4, mwaka huu kuhusu kuongeza umakini na usimamizi katika Sheria za Usalama Barabarani, leo nimeliagiza Jeshi la Polisi kuwa na mfumo wa Leseni za udereva utakaoweza kuwapunguzia alama madereva wanaofanya makosa yenye kuhatarisha usalama na uhai barabarani.”

Wakati Rais akitoa agizo hili, kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura alifanya
uhamisho wa aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Naibu Kamishna wa Polisi, Ramadhani Ng’anzi, kufuatia ongezeko la ajali za barabarani zilizoshuhudiwa mwezi Desemba, 2024 na alimteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, William Mkonda, aliyekuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Hata hivyo pamoja na hatua hizo zote tunaona haisadii kubadilisha viongozi wa usalama barabarani bali hatua kubwa zaidi zichukuliwe ili jamii na madereva wahisi adhabu zinazotolewa zina athari kwao.

Maoni yetu tunaona ipo haja ya madereva hawa kufungiwa maisha kwa kusababisha ajali hizi ili wasirudi barabarani
tena iwe fundisho kwa kila dereva ili waongeze umakini wanapokuwa katika safari mbalimbali.

Tunaamini adhabu ya kufungiwa maisha itawadhibiti vilivyo kwa sababu maisha ya watu yanapotea kizembe
barabarani, adhabu ziende mbali zaidi kama alivyoagiza rais na ziende mbali zaidi mtu atafute kazi nyingine ya kufanya kuliko kurudi barabarani kwa makosa ya uzembe kama haya.

Lakini pia rushwa imekuwa tatizo na imechangia ajali hizi, tunasema idhibitiwe maana zipo taarifa baadhi ya askari
wa usalama barabarani wanahongwa na kuachia madereva wa malori na mabasi kuendesha kwa kasi wanayoitaka kwa gharama za uhai wa watu wengine.

Vile vile suala la ushindani wa kibiashara umechangia pia kupoteza maisha ya watu wengi barabarani kwa sababu ya
sifa tu za mabasi kutambiana mabasi gani yanawahi kufika mwisho wa safari na matokeo yake imechangia ajali nyingi barabarani.