Kila mmoja ashiriki kikamilifu utekelezaji Mpango wa Nne wa Maendeleo

SERIKALI juzi iliwasilisha bungeni Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027 –2030/2031 unaotarajiwa kugharimu Sh trilioni 477.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo pia aliwasilisha Mpango Elekezi wa
Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027.

Kwa mujibu wake, Sh trilioni 477 ni fedha zitakazohitajika kuwekezwa katika sekta za kimageuzi na vichocheo vya ukuaji wa Uchumi, ukiwamo usafiri fungamanishi, nishati na uchimbaji, viwanda na biashara, kilimo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), mazingira na uhimilivu wa tabianchi, huduma za kijamii na maendeleo ya watu, utawala na utumishi wa umma pamoja na utafiti na maendeleo.

Amefafanua kuwa vyanzo vikuu vya rasilimali za kugharimia mpango huu ni sekta binafsi na sekta ya umma kwa uwiano wa 70:30.

Shabaha kuu za mpango zimetajwa kuwa ni kukuza pato halisi la taifa kwa asilimia 10.5; kuongeza Pato la Taifa kufikia wastani wa Dola za Marekani bilioni 118.1 na pato la mtu mmoja kufikia Dola za Marekani 1,638 ifikapo mwaka 2031.

Mpango huo umewasilishwa wakati Tanzania ikijiandaa kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo imebeba mambo makubwa sita, hivyo mpango huo wa miaka mitano utakuwa ramani ya utekelezaji wa Dira 2050.

Tumefarijika na jinsi serikali ilivyojipanga katika utekelezaji ikiwamo kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani huku ikijiandaa kuanzsha Mfuko wa Akiba wa Taifa chanzo chake kitatokana na sehemu ya mapato itokanayo na maliasili za taifa yakiwamo mafuta, gesi, dhahabu na madini mengine.

Aidha, kikubwa kingine ni kwamba utajikita katika kuongeza mapato ya kodi, eneo jingine ambalo Serikali ya Awamu ya Sita imefanya vizuri tangu iingie madarakani hivyo kuwezesha kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.

Kwa msingi huo, ni vyema Watanzania wakafahamu kwamba wanalo jukumu kubwa la kufanya kuhakikisha utekelezaji huo wa Mpango wa Nne wa Maendeleo unafanikiwa, na hivyo kutimia yale yanayokusudiwa.

Tunaamini kila mmoja kuanzia kwa watendaji hadi wananchi wa kawaida wakishiriki kikamilifu katika utekelezaji hakuna kitu kitakwama hasa kutokana na ukweli kuwa nia ya mpango iko wazi ikiwamo kukuza pato la mtu mmojammoja na pia kuchochea uzalishaji wa ajira kwa vijana.

Kwa jinsi ambavyo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imesimamia mambo mengi mazito na kuyafanikisha, hatuna shaka huu mpango utakapofikia ukomo, utakuwa umeleta matunda makubwa kwa Watanzania.

Tuunganishe nguvu kufanikisha hayo tukizingatia umoja wetu ndio nguvu yetu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button