‘Ajira mpya haziwezi kutolewa kwa uwiano sawa kila jimbo’

DODOMA; SERIKALI imesema nafasi za ajira mpya haziwezi kutolewa kwa uwiano sawa kwa kila jimbo.
Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Vijijini Flatei Massay aliyehoji kwa nini Serikali isipeleke ajira kwenye ngazi ya Halmashauri, ili kuweka uwiano wa nafasi katika kila jimbo.
“Kwa Mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2008, Toleo la 2 Aya ya 4.2, nafasi za ajira hutolewa kwa ushindani na kwa kuzingatia sifa stahiki kwa mujibu wa miundo ya maendeleo ya utumishi ya kada husika.
“Vilevile mgawanyo wa nafasi za ajira mpya katika utumishi wa umma huzingatia mahitaji ya watumishi yaliyoainishwa na mwajiri na kisha kuidhinishwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Ikama na Bajeti kwa mwaka wa fedha husika.
“Baada ya Ofisi ya Rais Utumishi kuidhinisha kibali cha ajira mpya, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma huendesha usaili wa kuwapata watainiwa stahiki na kisha kuwapangia katika maeneo yenye uhitaji ili kujaza nafasi wazi kulingana na mahitaji ya mwajiri kwa mwaka husika.
“Kwa msingi huo nafasi za ajira mpya haziwezi kutolewa kwa uwiano sawa kwa kila jimbo,” amesema Naibu Waziri.



