Akiba ya dhahabu BoT yafikia tani 6

GEITA: WIZARA ya Madini imeweka wazi kuwa hadi kufikia Julai 2025 Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ina hifadhi ya tani 6.84 ya dhahabu yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 682 tangu ilipoanza kununua dhahabu.
Naibu Waziri wa Madini Dk Steven Kiruswa alitoa taarifa hiyo Julai 06, 2025 katika hafla ya kufunga mafunzo ya kukuza ujuzi kwa wafanyakazi (wachimbaji wadogo) migodini mkoani Geita iliyofanyika mjini Geita.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu ikiwa ni utekelezaji wa programu ya kitaifa ya kukuza ujuzi na mnyororo wa thamani katika sekta ya madini.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Alana Nchimbi
Dk Kiruswa amesema hatua hiyo imeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 zenye hifadhi ya dhahabu iliyosafishwa barani Afrika ambayo ni kama mbadala wa fedha wa fedha za kigeni.
“Mchango wa sekta hii kwa pato la taifa umeendelea kukua na kuimarika, kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023/24 na kufikia asilimia 10 kwa mwaka huu wa fedha.
“Aidha sekta ya madini imefanikiwa kuchangia katika mfuko mkuu wa serikali kiasi cha Sh Trillioni 1.07 katika mwaka wa fedha 2024/25”, amesema.
Amesema dhamira ya mafunzo ya nadharia na vitendo kwa wachimbaji wadogo ni kuongeza mchango wao kufikia wachimbaji wa kati hadi kufikia wachimbaji wakubwa ambapo alisisitiza washiriki wote kuzingatia mafunzo.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Geita (GEREMA), Titus Kabuo
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Alana Nchimbi amesema mwaka 2024/25 serikali ilitenga sh bilioni 10.8 kufanikisha programu ya ujuzi ambapo wachimbaji 10,786 wamenufaika ikiwemo 479 kutoka Geita.
“Lengo la mafunzo ni kuongeza uwezo wa wachimbaji wa wadogo ili wafanye kazi kwa ufanisi, usalama na tija zaidi ili kuongeza uzalishaji, usalama mahala pa kazi, uelewa wa masuala ya kisheria na sera pamoja na soko la uhakika”.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya Wachimbaji Wadogo Nchini (Femata), Rodgers Senzero amesema mchango wa sekta madini umechangiwa na sheria ya madini kuruhusu malipo ya leseni kufanyika kwa shilingi.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo mkoani Geita (GEREMA), Titus Kabuo ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuongeza fursa ya leseni, mikopo na ujuzi kwa wachimbaji wadogo mkoani Geita.
Kabuo amewaomba wachimbaji wadogo kuiunga mkono serikali kwa kufuata sheria za madini na kukemea utoroshaji wa madini ili kuongeza mnyororo wa thamani ya madini nchini.