Akwilapo: Watumishi wasiwe sehemu ya migogoro ya ardhi
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo amesema wizara yake haitaki watumishi wa sekta ya ardhi kuwa sehemu ya migogoro ya ardhi nchini.
Dk Akwilapo alitoa kauli hiyo wilayani Masasi wakati alipowasili na kupokewa kwa mara ya kwanza tangu ateuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

“Kuanzia sasa hatutaki mtumishi wetu awe sehemu ya tatizo, tukigundua wewe mtumishi wa sekta ya ardhi umekuwa sehemu ya tatizo basi wewe si mfanyakazi wetu na hilo tutalisimamia,” alisema.
Alisema kuwa matatizo ya ardhi yapo na yanatengenezwa na watumishi wa sekta ya ardhi pamoja na wananchi. Ameweka wazi kuwa matatizo yaliyotengenezwa wizara yake itayatatua.

“Hatupendi kufukuza kazi watumishi maana tunajua kila mfanyakazi anategemewa na kumfukuza itakuwa kitu cha mwisho lakini kuna mahali inabidi sheria ifuate mkondo wake,” alisema.
Dk Leonard Akwilapo yupo wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara ambapo pamoja na mambo mengine atakutana na wananchi wa jimbo lake kwa lengo la kusikiliza na kizitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali jimboni humo.



