Amani, demokrasia vyatajwa ufanisi Mpango Maendeleo

DODOMA; SERIKALI imesema ufanisi wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2026/27 utajengwa katika misingi mbalimbali ikiwemo kuendelea kuwepo kwa demokrasia, amani, usalama na utulivu wa ndani na katika nchi jirani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof Kitila Mkumbo, ametoa kauli hiyo bungeni leo akiwasilisha nyenzo tatu zitakazowezesha kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Nyenzo hizo ni Mpango Elekezi wa Muda mrefu wa miaka 25 (2026/27 hadi 2050/51), Mpango wa Nne wa Maendeleo wa miaka mitano (2026/27 hadi 2030/31) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2026/27.

“Ufanisi wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2026/27 utajengwa katika misingi ifuatayo:

“Kuendelea kuwepo kwa demokrasia, amani, usalama na utulivu wa ndani na katika nchi jirani, inayowezesha shughuli za kiuchumi na uwekezaji kustawi.

“Kudumisha misingi ya utawala bora na utawala wa sheria, ikiwa ni pamoja na uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma; kuendelezwa kwa miundombinu ya nishati na usafiri na usafirishaji, sambamba na matarajio ya Dira 2050 ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara, viwanda na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Kuimarika kwa ubunifu na matumizi ya teknolojia za kidijitali katika huduma za kijamii na uzalishaji.

“Utekelezaji wa mageuzi ya kitaasisi na kiutawala chini ya falsafa ya 4Rs, unaolenga kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji; kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji kupitia mashirikiano ya sekta binafsi (PPP) na ushirikiano wa kikanda (EAC na SADC).

“Kuendelea kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili na yasiyo ya asili ikiwemo ukame, mafuriko, vita, milipuko ya magonjwa na misukosuko ya kiuchumi ya kimataifa kupitia mikakati ya kukabiliana na kupunguza athari zake.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button