Amani iwe mtaji muhimu wa maendeleo 2026

MWAKA Mpya 2026, ndio umeanza ikiwa ni siku ya pili tangu Watanzania walipoungana na watu wengine duniani kuupokea mwaka huo. Kwanza tunamshukuru Mungu kuwezesha wengi wetu kuuona mwaka na uwepo wetu ni dhamana kubwa kuhakikisha tunailinda Tanzania iendelee kuwa mahali pazuri na salama pa kuishi sasa na baadae.

Ikiwa ni siku ya pili leo, mwelekeo wa mwaka 2026 kwa kuangalia hotuba za viongozi wa serikali na dini katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, inaonesha ni mwaka wa kudumisha amani, umoja, haki na mshikamano ili kupata maendeleo na ustawi wa jamii.

Juzi akihutubia taifa akiwa Ikulu ndogo ya Tunguu, Unguja, Rais Samia Suluhu Hassan alisema serikali imejipanga kujenga umoja wa kitaifa na tayari hatua za kuunda Tume ya Maridhiano zimeanza. Rais Samia aliwahakikishia Watanzania kuwa serikali itashirikiana na wadau wote katika kukubaliana kuhusu muundo wa tume, aina ya wajumbe, majukumu yao na muda wa kazi hiyo na hatua hii tunaamini ni mwendelezo wa kudumisha amani.

Mbali na hilo, Rais Samia aliwasihi watanzania wasikubali tofauti za kiitikadi au kimtazamo ziwagawe na kuwapotezea malengo yao ya maendeleo na ustawi wa taifa kwani tofauti ni sehemu ya demokrasia, lakini hazipaswi kutumika kuigawa nchi. SOMA: Viongozi wa dini wahamasisha amani 2026

Ameeleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni moja tu na ndani ya jamhuri hiyo kuna Watanzania ambao wamejengwa na itikadi ya kuamini kwamba amani, umoja na mshikamano hujenga uzalendo na ndio virutubisho vinavyoiletea maendeleo endelevu na ustawi wa Watanzania. Aidha, viongozi mbalimbali wa dini katika mikesha ya Ibada za Mwaka Mpya katika ibada mbalimbali, walikazia amani na umoja kama msingi wa ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.

Ni wazi kauli za viongozi hawa zinatoa taswira ya wazi kuwa, amani ndio msingi wa kila kitu hivyo tunaungana nao kuwahimiza Watanzania kuilinda bila kuchoka tena kwa wivu mkubwa mwaka 2026. Katika mchanganyiko wa watu kama ilivyo kwa Tanzania kuwa na zaidi ya makabila 120, ni wazi watu wanakuwa na itikadi, mitazamo tofauti lakini kama alivyoagiza Rais Samia katika hotuba yake hiyo ya Mwaka Mpya, tofauti hizi zinapaswa kuwa chachu ya kulinda amani na si kuligawa taifa.

Tunaendelea kuhimiza Watanzania kufanyia kazi wito huu wa viongozi wa nchi na dini kuiombea nchi amani ili kupata nafasi kufanya shughuli za maendeleo bila bugudha na hivyo kukuza kipato cha mtu mmojammoja, kaya, jamii na taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button