Amani, umoja viwe msingi wa maisha kwa kila Mtanzania

ILI taifa lolote lipate maendeleo, kuna mambo ya msingi yanayopaswa kuzingatiwa, ikiwemo uwepo wa amani na utulivu.

Amani katika nchi inachochea ustawi wa jamii kwani huvutia wawekezaji, watalii na kuchochea maendeleo kwa kuwa watu hupata muda wa kufanya kazi bila hofu na hata kiimani kwa sababu ya kunakuwa na uhuru mkubwa wa kuabudu.

Tanzania ni miongoni mwa nchi inayoendeshwa kwa kuzingatia misingi ya haki, amani na utu, tunu ambazo zimejengwa na waasisi wa taifa na kuwekewa misingi ya kizalendo.

Kutokana na ukweli huu, Watanzania wanapaswa kuendeleza tunu hizo kwa kuhakikisha amani inakuwa msingi wa kuwa na maisha bora miongoni mwao na kuakisi nuru hiyo njema kikanda na duniani kote.

Msisitizo wa kutunza amani ni jambo linalopaswa kuzama kwenye mioyo, akili na mawazo ya kila raia wa Tanzania na hili limesisitizwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, taasisi na mashirika mengi yasiyo ya kiserikali.

Kwa mfano, Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) juzi likizungumza na gazeti hili limewaomba viongozi wa dini kuwaongoza Watanzania kufanya dua, sala na maombi kwa Mungu awape faraja na amani.

Aidha, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi juzi aliposhiriki katika sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Malindi, Unguja aliwahimiza wananchi na viongozi wa dini kuendeleza utaratibu wa kuiombea nchi amani ili idumu.

Jana, Mkutano Maalumu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya mtandao ukihusisha viongozi wakuu wa nchi wanachama, mbali na kuwapongeza marais wa ukanda huo walioshinda uchaguzi katika nchi zao akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, walisisitiza umuhimu wa ushirikiano na amani katika ukanda huo.

Msisitizo huu wa amani ni taswira ya wazi kuwa amani ni msingi wa kila kitu na kuwa nayo ni jambo moja na kuitunza ni jambo jingine linalohitajika kutekelezwa na jamii husika.

Tunawakumbusha Watanzania kujirudi, kujitafakari na kuchukua uamuzi ulio bora zaidi wa kuchagua amani kuongoza maisha ya kila siku.

Tunashauri hivyo kwa sababu katika vurugu zilizotokea siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, baadhi ya mali za umma na watu binafsi na maisha ya watu yalipotea na kwa muda mfupi katika maeneo zilikotokea, hali haikuwa shwari.

Ni muhimu kuzingatia misingi ya amani kuifanya Tanzania daima ibaki kuwa eneo zuri la kuishi, kuwekeza na kutembelea, huku tukiangalia zaidi kesho yenye ustawi na kutumia mazungumzo kama ilivyo hulka ya Watanzania kutatua changamoto.

Tanzania ya amani inawezekana.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button