Ambindwile aahidi mikopo riba nafuu Iringa Mjini

IRINGA: Mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wakili Moses Ambindwile, amezindua ajenda yenye mvuto mkubwa kwa wananchi wa Iringa Mjini kwa kuahidi kuanzisha Jimbo Saccos itakayotoa mikopo isiyo na riba pamoja na Trust Fund kwa ajili ya kusaidia makundi maalumu kama wajane, yatima, watu wenye ulemavu na wanawake waliotelekezwa.
Akizungumza katika mkutano wa kuomba ridhaa kwa wajumbe wa CCM Kata ya Gangilinga, Kitanzani, Mshindo na Mivinjeni, Ambindwile amesema amejipanga kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi kila siku, ikiwemo kukosekana kwa mikopo rafiki kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.
“Mikopo inayotolewa na halmashauri siyo rafiki kwa wananchi. Nitahakikisha asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotakiwa kuwafikia wananchi kwa njia ya mikopo, inatolewa kwa uwazi na kwa manufaa ya wengi. Najua wengi hawajanufaika, nitalisimamia hilo ipasavyo,” alisema Ambindwile.
Amefafanua kuwa Jimbo Saccos hiyo itawalenga watu wa kipato cha chini na wa kati wanaojishughulisha na biashara ndogondogo na shughuli za kijamii.
“Mikopo hii itatolewa bila riba au kwa riba nafuu kabisa, itakayolipika bila kuwatesa,” aliongeza.
Mbali na hilo, amebainisha mpango wa kuanzisha Trust Fund ya Jimbo kwa ajili ya kugusa maisha ya watu wanaoishi katika mazingira magumu kama wajane, yatima na watu wenye ulemavu.
Katika hatua nyingine, Ambindwile ameahidi kuanzisha dawati maalumu la msaada wa kisheria katika ofisi ya mbunge, litakalokuwa likitoa huduma bila malipo kwa wananchi wote watakaohitaji msaada wa kisheria, hususan katika migogoro ya kifamilia, ardhi na mikataba.
“Mawakili nitawaweka ofisini kwa ajili ya kuhudumia kundi hilo. Wanawake na watoto wanaonyanyaswa hawatabaki kimya. Nitahakikisha wanapata msaada wa kisheria na wahusika wanawajibika,” alisema kwa msisitizo.
Aidha, ameeleza dhamira yake ya kutoa elimu ya uchumi na fedha kwa wananchi ili kuwawezesha kujinasua kutoka kwenye utegemezi na kujiendeleza kiuchumi.



