TAASISI ya Kuboresha Mifumo ya Masoko Tanzania (AMDT), imeahidi kuendeleza ubia wa kuzalisha mbegu za alizeti nchini ikiwa ni pamoja na kuweka miundombinu ya umwagiliaji ili mbegu hizo zizalishwe mara mbili au tatu kwa mwaka.
Mtendaji Mkuu wa AMDT, Charles Ogutu amesema hayo katika ziara aliyoambatana na wafanyakazi 15 walipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Ilonga Kilichopo Kilosa, Morogoro kujionea maendeleo ya uzalishaji wa mbegu.
Ogutu amesema wameingia ubia wa uzalishaji wa mbegu katika kituo cha Ilonga kwa kuwa unachangia kitaifa kuwa na usalama wa mbegu, pia mbegu hizo baada ya kuzalishwa na kuthibitishwa zikifika kwa mkulima zitaongeza tija katika uzalishaji.
” Ubia huu pia unasaidia Watanzania wengi ambao ni wakulima wa alizeti kuongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa na kipato, kwani wengi wanapata ajira uzalishaji unapokuwa mkubwa kwa kuwa viwanda vinavyosindika zao la alizeti vinaongezeka,” amesema.
Amesema mchango wa ubia huo umeongeza upatikanaji wa mbegu, kwani msimu uliopita waliwezesha sekta binafsi kupitia TARI Ilonga kuzalisha tani 40 pamoja na changamoto ya mvua iliyokuwepo, hivyo matarajio yao kwa msimu huu wanategemea kupata sio chini ya tani 100.
” Tunategemea ubia huu wa uzalishaji mbegu utaendelea na msimu unaofuata, na tutaangalia maeneo mengine ambayo tutaweza kushirikiana hata ikiwezekana kuzalisha mara mbili au tatu kwa mwaka,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha TARI Ilonga, Emmanuel Chilagani ameshukuru kwa ushirikiano huo na kuomba wadau hao kuangalia eneo la miundombinu ya umwagiliaji ili uzalishaji uongezeke kwa mwaka badala ya kutegemea mvua.
“Tuendelee kushirikiana, sasa hivi kituo kinategemea mvua katika uzalishaji wa mbegu, huu sio mfumo mzuri sana kwa sababu tunazalisha mara moja kwa msimu. Tukipata mfumo mzuri kupitia serikali na wadau itasaidia sana kwa mwaka moja kuzalisha zaidi ya mara moja na kuokoa hasara inayotokana na uhaba wa mvua,” amesema.
Naye Meneja wa Mradi kwa ubia kati ya AMDT na TARI, ambaye pia ni Mratibu wa Alizeti Kitaifa, Frank Reuben amesema kwa kuwa kwa miaka mingi uendelezaji wa alizeti haukuwa mkubwa serikali imeamua kuwekeza katika zao hilo na kulifanya kipaumbele.
” Kama TARI tuliona ni vyema kushirikiana na wadau ili kuleta ule ubia kati ya serikali na sekta binafsi hasa kwenye uzalishaji wa mbegu,”amesema.
Amesema TARI Ilonga iliandika maandiko kwenda kwa mfadhili AMDT yakilenga kupata fedha ambazo wanapozipata wanawapa kampuni za uzalishaji mbegu na kuziuza kwa wakulima, kiasi kidogo cha fedha wanabaki nacho kwa ajili kufanya uzalishaji.