Amos jela miaka mitatu kwa kung’ata watu

MWANZA: MAHAKAMA ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, imemhukumu kifungo cha miaka mitatu jela, Mkazi wa Kijiji cha Soswa wilayani humo, Amos Malaki ,30, baada ya kupatikana na hatia ya kuwajeruhi watu wawili kwa kuwang’ata.
Katika taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imeeleza baada ya mshtakiwa kutenda kosa hili alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na alikiri kutenda makosa hayo bila kuisumbua mahakama.
Amosi alimng’ata Regina Thomas katika jicho lake na Mashaka Daudi kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kulia.
Akisoma shtaka hilo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nyamhanga Tissoro ameeleza kuwa tukio la kwanza lilitokea Januari 8, 2025, majira ya saa tano usiku, ambapo mshtakiwa alimg’ata Regina Thomas. Tukio lingine lilitokea Januari 9, 2025, saa 6:01 usiku, ambapo alimg’ata Mashaka Idd Daudi, aliyekuwa akijaribu kutatua ugomvi.
Mahakama ilitumia ushahidi wa PF3 kutoka kwa wahanga baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu, pamoja na maelezo ya kukiri ya mshtakiwa aliyoyatoa wakati akihojiwa na Polisi, na kuamua kumtia hatiani kwa makosa hayo.
Hata hivyo mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea, mshtakiwa alieleza kuwa pombe ilichangia kutokea kwa makosa hayo, na kwamba mhanga wa pili aliingilia ugomvi usiomhusu.
Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, Hakimu Kisoka alimhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka mitatu jela, huku akisema kuwa iwe ni fundisho kwa watu wenye tabia kama ya Amos.



