Mahakama kutoa amri J’tatu ushahidi ‘live’ kesi ya Lissu

DAR ES SALAAM; MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema Agosti 18,2025 itatoa amri kuhusu kurushwa mubashara kwa maelezo ya mashahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Pia katika tarehe tajwa mahamakama hiyo inatarajiwa kusikiliza maelezo ya mashahidi pamoja na idadi ya vielelezo vitakavyotumiwa katika shauri hilo wakati wa usikilizwaji wake.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga amesema hayo leo Agosti 13,2025 mahakamani hapo shauri hilo lilipopelekwa kwa ajili kujua hali la shauri hilo na kutoa uamuzi wa yaliyojiri katika kikao cha mahakama kilichopita.
Hatua hiyo imefuatia uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu wa Agosti 4,mwaka huu wa kubariki taarifa za mashahidi ambao ni raia katika kesi hiyo kulindwa kabla ya kupeleka taarifa mahakama kuu kwa ajili ya kuendelea ili kulinda usalama wao.
Awali, Wakili wa serikali Mkuu, Nassoro Katuga ameeleza mahakama kuhusu uamuzi huo uliotolewa tarehe tajwa ambao ulitoa amri sita ikiwemo vyombo vya habari kutoruhusiwa kutangaza mubashara taarifa za mashahidi ambao ni raia wakati wa kusoma maelezo ya mashahidi na ushahidi wakati wa usikilizŵaji wa kesi
Akiwasilisha hoja hiyo mbele ya mahakama hiyo wakili Katuga alidai ingawa Mahakama Kuu imeruhusu matumizi ya mashahidi wa siri, bado kuna haja ya kuweka zuio la kurusha mwenendo wa kesi mubashara wakati wa ushahidi wa mashahidi hao.
Katuga amedai kuwa kurusha mwenendo huo moja kwa moja ni sawa na kufanya uchapishaji wa ushahidi, jambo ambalo litakuwa kinyume na amri ya Mahakama inayolenga kulinda usalama na utambulisho wa mashahidi hao.
Anaongeza kwa kuwa ushahidi huo utatolewa kwa namna ya siri, kuwepo kwa matangazo ya moja kwa moja kunaweza kusababisha mashahidi kutambulika kupitia maelezo yao, hivyo kuhatarisha ulinzi wao.
Baada ya kuelezwa hayo Lissu amepinga akidai uamuzi uliotolewa na Jaji Hussei Mtembwa kufunika mambo mengine ambayo hayajakatazwa.
Kuhusu hoja ya kwamba kesi isiwe mubashara , Lissu alidai kuwa ni hoja ambayo haijaamuliwa na Jaji yeye kasema amekataza kile ambacho kitamfichua shahidi, akisisitiza uamuzi wa jaji Mtembwa ilisema utambulisho wao hautatolewa hadharani pamoja na anuani za makazi yao.



