Anangisye atoa madini kwa wahitimu

DAR ES SALAAM: MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye amewataka wahitimu kutumia elimu kubwa walioipata kuleta ushawishi chanya kwa watu wote wanaowazunguka kwani elimu walioipata ni mali ya Umma hivyo basi elimu lazima ilete faida.

Aidha amewataka wahitimu wawe wazalendo kwa nchi yao kwani watu wengi wanatarajia mengi kutoka kwao “hakuna mtu mwenye akili timamu asiyetambua mchango wa vijana wanaojitambua katika kuendeleza familia, jamii na taifa lao”.

Hayo yamesemwa wakati wa Mahafali ya 53 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.

Prof. Anangisye amewaeleza wahitimu kuwa endapo ajira serikalini au katika sekta binafsi zitachelewa kupatikana wawe wepesi kuangalia sehemu nyingine ambapo maarifa na ujuzi wao unaweza kutumika kwa ufanisi zaidi.

Pamoja na hayo amesema kuwa ndani ya mwaka mmoja chuo hicho kimepiga hatua muhimu ya maendeleo ikiwemo kuandaa kongamano la kwanza la kiswahili nchini Ghana lililofanyika kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ghana-Legon.

Amesema kuwa kwenye mafanikio hayo pia chuo kimefanikiwa kukamilisha ujenzi wa jengo la kutolea huduma katika kituo cha Afya ili kuwapatia wanajumuiya ya chuo huduma bora za afya.

Ameeleza kuwa chuo kimeendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuendeleza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania ambapo chuo kilisaini mkataba wa makubaliano wa kufundisha kiswahili na Chuo Kikuu cha Havana kilichoko Cuba.

Habari Zifananazo

Back to top button