Anayedaiwa kumuua ‘trafiki’ kuhukumiwa Machi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Machi 17, 2023 kusoma hukumu ya kesi ya mauaji ya askari wa kikosi cha usalama barabarani, Sajenti Mensah inayomkabili Amani Philipo.

Tarehe hiyo ilipangwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Lumuli Mbuya anayesikiliza kesi hiyo baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wake.

Akihitimisha ushahidi wake huku akiandamwa na kilio na kwikwi, shahidi namba mbili, Samuel Thomas aliieleza mahakama jinsi alivyokuwa na mshitakiwa siku anayotuhumiwa kufanya tukio na yeye kujumuishwa katika kesi hiyo.

Akiongozwa na mawakili wa kujitegemea, Hassan Kiangio na Selemani Almasi shahidi huyo alidai kuwa Julai 22, 2016 siku ambayo Amani anatuhumiwa kutekeleza mauaji alikuwa naye toka asubuhi hadi saa 4:00 usiku.

Alisema yeye siku hiyo akiendesha gari la Spacio walitoka Tangi Bovu saa tatu na nusu usiku ambako walikunywa bia kidogo kisha yeye na Amani wakaondoka kwenye baa ambayo inamilikiwa na mtu aliyemtaja kwa jina la Michael.

Alidai alimfikisha Amani kwake Mbezi Africana saa nne usiku na yeye kuelekea kwake Tegeta na kumsisitiza Amani waonane siku inayofuatia kwa ajili ya kutekeleza azma yao ya kuchoma nyama.

Samuel alidai siku iliyofuata Julai 23, 2016, saa nne asubuhi alipigiwa simu na Amani na kuulizwa kama yupo nyumbani na alipomjibu kuwa yupo akamwambi kuwa yeye yupo getini anaomba amfungulie.

Alidai alipokwenda kufungua geti alishangaa kuona aliyeingia hakuwa Amani bali askari aliyejitambulisha kwa jina la Ben Magufuli na kumuuliza mahala alikokuwa na Amani jana yake.

Alidai alimweleza safari yao iliyowafikisha Muhimbili hadi baa na kisha kumrejesha nyumbani saa nne usiku.

Alisema askari alimtaka aseme ukweli ili amsaidie Amani kwani ana matatizo, akamuuliza matatizo gani? Hakumjibu bali akatoka naye nje ya geti ambako alimkuta Amani akiwa na kijana aliyemtaja kwa jina la Oswald Mang’ombe huku wamefungwa pingu.

“Nilimuuliza Amani nini kinaendelea? Amani akajibu hata mimi sijui kwani wamekuja kunikamata tu nyumbani,” alisema.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button