Anayetuhumiwa kutakatisha Sh bil 1.5 asomewa mashtaka 106
MFANYABIASHARA Gastom Danda maarufu James, mkazi wa Mbezi Beach Dar es Salaam, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu akikabiliwa na mashtaka 106 ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha haramu zaidi ya Sh bilioni 1.5.
Danda alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Adolph Velandumi akishirikiana na Yusuph Aboud mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo huku yeye akiwakilishwa na Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), Edward Hosea.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na mawakili hao kwa kupokezana, ilidaiwa kuwa katika mashtaka ya kughushi mshtakiwa huyo alighushi barua za utambulisho za wafanyakazi 36 waliodaiwa kuwa ni wa kampuni ya uchimbaji madini ya Savanna sambamba na kughushi fomu za maombi ya mkopo kwa kutumia majina ya wafanyakazi hao.
Ilidaiwa kwa kughushi huko mshtakiwa alijipatia zaidi ya Sh bilioni 1.5 kwa njia ya udanganyifu akionesha wafanyakazi hao waliomba mikopo kutoka kwa benki ya CRDB Msasani, ambayo ilikuwa ni ya viwango tofauti kati Sh milioni 34 hadi milioni 50 kwa kila mmoja.
Ilidaiwa kwa makosa tangulizi ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu mshtakiwa alitakatisha fedha haramu Sh 1,569,600,000.
Mshtakiwa huyo alidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti na Novemba, 2020 katika benki ya CRDB tawi la Msasani mkoani Dar es Salaam.
Mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi inayomkabili.
Upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na uliomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Mshtakiwa alipelekwa mahabusu kwa kuwa shtaka la utakatishaji fedha haramu halina dhamana
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 22, 2022.