MWANAUME mmoja aliyefahamika kwa jina la Kisado amekwepa kifo mikononi mwa wananchi, baada ya kudaiwa kufanya mazingaombwe ambayo yalisababisha wanafunzi wa Shule ya Msingi Town, Manispaa ya Tabora kuonekana kama wamepata mapepo.
Tukio hilo limetokea jana ambapo mashuhuda wamesema Kisado aliwamwagia maji wanafunzi darasani na kusababisha kutokea kwa hali hiyo.
Baada ya kuwamwagia maji, wanafunzi walianza kukimbia hovyo, na baadhi yao walionekana wakipandisha mashetani, hali iliyozua hofu kubwa.
Zainabu Chonanga mmoja wa mashuhuda amesema kuwa watoto walishindwa kutulia licha ya kuombewa kwa muda. Hali hiyo ilisababisha wazazi na walezi kufurika shuleni na kudai Kisado achukuliwe hatua.
Kisado alilazimika kurudi shuleni baada ya kupigiwa simu, na alipofika, Mwalimu Mkuu alilazimika kumfungia ofisini kwa ajili ya usalama wake, baada ya wazazi kuanza kuhamaki. Askari Polisi walifika usiku na kumchukua Kisado, Mwalimu Mkuu na baadhi ya wazazi hadi kituo cha polisi kwa mahojiano.
Mtendaji wa Kata ya Gongoni, Mzelela Kalamata, amesema anafuatilia tukio hilo ili kubaini undani wake, huku Diwani wa Kata hiyo, Kessy Abdurahmani, akisema tukio hilo ni la kipekee katika kata yao na kuwaomba wazazi kuwa watulivu wakati wakifuatilia uchunguzi.