AQRB yasisitizwa malengo yanayopimika

ARUSHA: Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, ameitaka Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) kuandaa mpango mahsusi utakaobainisha mchango wa taaluma za usanifu majengo na ukadiriaji majenzi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kasekenya amesema mpango huo unapaswa kuwa na malengo na viashiria vinavyopimika ili kuhakikisha mchango wa wataalamu wa sekta ya ujenzi unaonekana katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa.

Ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Sita wa AQRB (AQ’26) kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za Serikali, sekta binafsi na taasisi za elimu ili kuboresha sekta ya ujenzi nchini.

Amesema Wizara ya Ujenzi na taasisi zinazohusika zinapaswa kuimarisha uratibu wa usajili, utoaji wa vibali na ukaguzi wa miradi ya ujenzi ili kupunguza urudufu wa majukumu bila kuathiri usalama na ubora wa miradi.

Aidha, ameitaka AQRB, kwa kushirikiana na sekta binafsi, kuongeza fursa za Mpango wa Uzoefu wa Kitaaluma kwa Wahitimu (AQIP) na kuhakikisha wataalamu wazawa wanapata nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika utekelezaji wa miradi mikubwa nchini.

Amesisitiza pia umuhimu wa bodi hiyo kuimarisha ufuatiliaji wa maazimio ya mikutano yake, akibainisha kuwa taarifa alizopokea zinaonyesha utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa mwaka 2025 (AQ’25) umefikia asilimia 62.

Amesema bodi hiyo inapaswa kuongeza kasi ya utekelezaji wa maazimio yaliyobaki na kuhakikisha yanazaa matokeo yanayopimika katika kuboresha utendaji wa sekta ya ujenzi.

“Ninahitaji kuona utekelezaji zaidi na matokeo yanayopimika,” amesema Kasekenya akisisitiza uwajibikaji katika kutekeleza maazimio ya mikutano ya bodi hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button