Ashauri kusoma ujasiriamali

MWANAFUNZI Masha Sogoma (65), ameshauri wazee wenzake kusoma elimu ya darasani na ujasiriamali.

Masha ambaye ni mwanafunzi wa elimu ya Mpango wa Uwiano Kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (Mukeja), ametoa ushauri huo katika Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima Kitaifa yanayofanyika Kibaha mkoani Pwani.

“Ninawashauri wazee ambao hawajapata hii elimu waingie ili iwasaidie.

“Tumesoma baada ya kusoma tukawezeshwa tujifunze ujasiriamali ili tusikae tu bila kuwa na kitu cha kutuingizia kipato,” amesema.

Ameitaka serikali kuwatambua wazee wengi ambao wako vijiji ambao hawajafikiwa na elimu hiyo.

Amesema baada ya masomo anatengeneza bidhaa za batiki, sabuni, dawa ya kuchua, mafuta ya kupka pamoja na sabuni za mlonge.

Naye Mwalimu wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) pamoja na Kisomo chenye Manufaa na Mwendelezo (KCM), Rehema Gabriel amesema ana darasa la wazee kuanzia miaka 60 na kuendelea anaowafundisha katika kituo cha wazee kilichopo Shule ya Msingi Mwendapole A mkoani Pwani.

“Darasa lingine la Kisomo chenye manufaa na mwendelezo linapatikana eneo la CCM Wilaya ya Kibaha,” amesema.

Kwa maelezo yake wanafunzi wake hao wanaingia darasani wanajifunza KKK na stadi za kazi, baadae wanaingia darasani kwa ajili ya ujasiriamali.

Amesema wanafunzi hao wazee wanajifunza kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemomafuta, sabuni, batiki, mkaa, lishe, sabuni za usafi na nyinginezo nyingi.

Amesema darasa lake la wazee lililopo eneo la Shule ya Msingi Mwendapole A lina wanafunzi 72 ambalo limegawanyika katika madarasa mawili.

“Katika darasa hilo unawabembeleza wazee kama wanafunzi wa chekechea ili waingie darasani, na lile darasa lingine ni la wanafunzi waliosoma zamani ambao sasa tunawakumbushia,” amesema.

Amesema lengo la elimu ya wazee ni kutoa dhana iliyojengeka katika jamii kuwa mtu akishakuwa mzee hana maana.

“Uzee sio kuishia bali ni hazina tunachota hazina za wazee, kule ziliko na kuzileta huku,” alisema na kuongeza kuwa darasa lake lingine lina wazee 30.

Akizungumzia changamoto ameiomba walimu wa madarasa hayo ya wazee wapelekwe mafunzo badala ya kutuia uzoefu katika kufundisha, kwa kuwa mzee ni kama mtoto anahitaji kubembelezwa.

Naye Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Profesa Michael Ng’umbi amesema wajibu wao ni kuhamasisha jamii kuona elimu ya watu wazima bado ni nyenzo muhimu katika kujenga utu, kuhakikisha kwamba haki ya msingi ya binadamu ya kujua kusoma, kuandika na kuendelea kujifunza muda wote inazingatiwa.

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa taasisi hiyo upande wa taaaluma, utafiti na ushauri Dk Philip Sanga amesema elimu hiyo ya watu wazima umuhimu wake ni kukumbusha jamii kuhusu umuhimu wake.

“Elimu ya watoto tunasema inaandaa watoto kwa ajili ya maisha ya baadaye lakini wanapojifunza watu wazima ni kwa aajili ya kujifunza sasa,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button