‘Asilimia 21 wanafunzi la saba hawana ufaulu mzuri’

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk Charles Msonde

ASILIMIA 21 ya wanafunzi wa darasa la saba, wanamaliza bila kupata ufaulu wa kuwawezesha kujiunga na kidato cha kwanza.

Haya yalibainishwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk Charles Msonde wakati wa kutoa wasilisho kwa wakuu wa mikoa kwa lengo la kuwajengea uwezo ili wakaongeze kasi ya kusimamia sekta hiyo hususani katika utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Awali na Msingi.

Alisema eneo hilo ni kati ya maeneo sita yenye changamoto katika elimu ya awali na msingi kutokana na tathmini iliyofanywa na Ofisi ya Rais-Tamisemi.

Advertisement

Alisema eneo lingine ni msongamano mkubwa wa wanafunzi darasani na uchakavu wa miundombinu kwa baadhi ya shule.

“Tathmini iliyofanywa na Ofisi ya Rais Tamisemi katika eneo hilo inaonesha kuwa shule 10,804 kati ya shule za msingi za serikali 17,182, zina msongamano mkubwa ya wanafunzi zaidi ya 60 katika darasa moja na shule zisizo na msongamano ni 6,378,” alisema.

Dk Msonde alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, serikali imepanga kujenga vyumba vya madarasa zaidi ya 12,000 ikiwa ni wastani wa madarasa 3,000 kila mwaka na matundu ya vyoo ndani ya miaka mitano kupitia mradi wa BOOST.

Pia alisema kuna mdondoko wa wanafunzi wa elimu ya msingi ambao umeongezeka kutoka asilimia 0.89 mwaka 2020 hadi asilimia 1.8 mwaka 2021.

Dk Msonde alisema changamoto nyingine ni baadhi ya wanafunzi wanaomaliza darasa la kwanza na la pili bila kumudu stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.

Pia usimamizi dhaifu wa utekelezaji wa mitaala kwa baadhi ya viongozi na baadhi ya walimu kukosa ari na morali ya kufanya kazi.

Akifafanua zaidi kuhusu mradi wa BOOST, Dk Msonde alisema mradi huo ni wa miaka mitano kuanzia mwaka 2921/22-2025/26 na utagharimu Sh trilioni 1.15.

“Hizi ni fedha ambazo ni za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia, asilimia 0.4 zitatolewa kugharamia shughuli za mradi na asilimia 96 zitakuwa zinalipwa baada ya kufikia matokeo yaliyokubaliwa na ndio maana tumewapitisha kwenye mradi huu ili mkasimamie ipasavyo utekelezaji wa mradi huu,” alisema.

Dk Msonde alisema matokeo ya mradi huo ni kuwa madarasa 7,741 yatabomolewa na kujengwa upya, madarasa 35,914 yatafanyiwa ukarabati mkubwa, madarasa 65,015 yatafanyiwa ukarabati mdogo na madarasa 38,618 hayahitaji ukarabati kwa sasa.

Alisema pia kutakuwa na uwiano wa ufikishaji elimu ya awali kutoa asilimia 76.9 hadi asilimia 85, ongezeko la wanafunzi kubaki shuleni asilimia 66.2 na halmashauri zote 184 kuzingatia utawala bora.

Dk Msonde alisema kwa mafunzo ya walimu kazini ni kuwafikia zaidi ya asilimia 50 kwenye ngazi ya shule na vituo vya walimu, vifaa na mafunzo kwa walimu wa elimu ya awali na ununuzi na usambazaji wa vifaa vya Tehama kwenye shule zaidi ya 800.

“Pia kutakuwa na utekelezaji wa programu ya shule ya msingi salama katika shule za msingi zaidi ya 6,000,” alisema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *