Askari wa uhifadhi wafundwa kuhusu maadili
ASKARI wa Jeshi la Uhifadhi (JU) nchini wametakiwa kuzingatia uwadilifu na misingi ya jeshi hilo na kwamba askari yoyote atakayekiuka taratibu, kanuni na sheria hatua kali zitachukukiwa dhidi yake.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba amesema hayo wilayani Biharamuro mkoani Kagera, alipozungumza na uongozi wa Hifadhi ya Taifa Chato, na askari wa Jeshi la Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (TANAPA) na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Wakulyamba licha ya kuwapongeza askari hao kwa kazi nzuri wanazofanya, amesisitiza kuwa, uongozi wa wizara hiyo hauto mvumilia askari yoyote atakaekwamisha jitihada za wizara za usimamizi bora wa uhifadhi hususani katika kupambana na ujangili, mifugo ndani ya hifadhi na uchomaji moto misitu iliyohifadhiwa kisheria.
Katika hatua nyingine Wakulyamba amekutana na Kamati ya Ulinzi na usalama Wilaya ya Biharamuro na kuupongeza uongozi wa Wilaya hiyo kwa ushirikiano unaotoa katika uhifadhi wa Hifadhi ya Burigi Chato, na kuahidi kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Waziri Angellah Kairuki itaendelea kushirikiana vyema na uongozi wa wilaya hiyo.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya hifadhi ya Burigi Chato, Mkuu wa Hifadhi Burigi Chato, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ismail Omari Ismail, amesema ndani ya muda mfupi wa uongozi wake wamefaniliwa kupambana na uingizaji wa mifugo ndani ya hifadhi kwa asilimia 225 kutoka Januari 2022 – February 2023 kutoka mifugo 13,839 hadi 6, 154 kwa Januari 2023 – Februari 2024 na kuwa zoezi hilo ni lakudumu.
Aidha Ismail kwa niaba ya watumishi wengine ameahidi kufanyia kazi maagizo yote waliopewa na uongozi wa Wizara hususani kusimamia nidhani ya askari, kubuni njia mbalimbali za kiuchumi na kuimarisha mahusiano mema, na viongozi wa serikali ngazi ya mkoa hadi vijiji pamoja na wanchini waishio pambezoni mwa hifadhi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Biharamuro Advera Bulimba amesema hapendezwi kuona baadhi ya watu wanafanya shughuli za kijamii ndani ya hifadhi kama vile kilimo, uchomaji wa mkaa na ufugaji hivyo Kamati ya Ulinzi na Usalama chini yake itaendelea kushirikiana na wizara ili kutokomeza changamoto hiyo ili hifadhi hiyo iendelee kuwa neema kwa wanachi wa Biharamuro na Tanzania kwa ujumla.