Askofu Mdegela ahofia ongezeko la makanisa Iringa

ASKOFU Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, Profesa Owdenburg Mdegela, amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, kufuatilia kwa makini shughuli zinazofanywa na makanisa yanayomilikiwa na watu binafsi, ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi katika mji wa Iringa.

Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 30 ya Kituo cha Watoto Wenye Uhitaji Maalum cha Huruma, pamoja na kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi kwa watoto wa kituo hicho kinachomilikiwa na KKKT Dayosisi ya Iringa, Askofu Mdegela alitoa wito huo kwa viongozi na wananchi wa mkoa huo.

Katika mahubiri yake wakati wa tukio hilo, Askofu Profesa Mdegela alisema kuwa ongezeko la makanisa ya Kikristo katika mji wa Iringa limekuwa changamoto kwa jamii, kwani wananchi wengi wameyumbishwa na kujisahau umuhimu wa kujitolea kusaidia watu wenye uhitaji.

Advertisement

Badala yake alisema, fedha nyingi hutumika katika kuwatunza wachungaji wa makanisa hayo.

“Napenda kuwaambia Wakristo wenzangu kwamba utitiri huu wa makanisa hapa Iringa hauna tofauti na VIKOBA, ni sehemu ya watu kujipatia kipato kwa maslahi yao binafsi kutoka kwa waumini,” alisema Askofu Prof Mdegela.

Aliwahimiza Wakristo wajikite zaidi katika kujitoa kwa ajili ya wenye uhitaji na maskini kama sehemu ya sadaka na njia ya kuomba baraka kutoka kwa Mungu, badala ya kuhama hama madhehebu wakitafuta baraka.

Akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu, Dk Dotto Biteko, katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, aliwasihi wananchi wa Iringa kuwa na moyo wa kujitolea kwa ajili ya watu wenye uhitaji ili kujenga mustakabali bora wa kizazi kijacho.

Aliongeza kuwa, uwepo wa Kituo cha Huruma katika wilaya hiyo umekuwa msaada mkubwa kwa watoto waliotelekezwa na wazazi wao na ndugu zao, kwani kituo hicho kinawalea na kuwapatia mafunzo ya maadili.

Kupitia changizo la ujenzi wa shule hiyo, inayotarajiwa kugharimu Sh milioni 450, kiasi cha Sh 309,385,000 kilipatikana, ambapo Sh 119,873,800 ni fedha taslimu na ahadi ni Sh 189,511,200.

Miongoni mwa waliotoa michango yao ni pamoja na Naibu Waziri Mkuu mwenyewe aliyetoa Sh milioni 10, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas, aliyetoa Sh milioni tatu, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, aliyetoa Sh milioni moja, na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, aliyetoa Sh milioni 2.