ATC , RUWASA kuzalisha mita janja

CHUO cha Ufundi Arusha (ATC) kimesaini hati ya makubaliano na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhusu uzalishaji wa mita janja. Mita hizo zinaruhusu malipo kabla ya matumizi ya huduma za maji, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza baada ya kusaini hati hiyo, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Mussa Chacha alisema ATC ina majukumu matatu ikiwemo kufundisha, kufanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu ambapo eneo la utafiti ndilo limewafanya kuwa na uhusiano na Ruwasa.
Amesema Ruwasa walikuwa na changamoto ya kiutendaji ambapo walitaka wananchi wapate mita janja ambapo waliingia makubaliano ya kuanza kufanya utafiti wa miaka mitatu kwa pamoja ambapo mwishoni walipata mita ambazo zinafaa na zilizoboreshwa. SOMA: Wasiojulikana waiba mita za maji Kigoma Ujiji
Ameongeza kuwa tayari wananchi wana uelewa kuhusu mita hizo na kuna wananchi ambao tayari wanazitumia ambapo wamegundua kuwa zinafanya kazi vizuri kwa mazingira ya Kitanzania na ndiyo maana wakafikia hatua ya kuingia makubaliano na Ruwasa kwa ajili ya kuanza uzalishaji wa hizo mita kwa wingi.
“Sisi ATC tunawahakikishia Ruwasa kuwa teknolojia tunayo na wameshaithibitisha na uwezo wa kuzalisha pia tunao na ukiangalia chuo cha ufundi Arusha tuna wanafunzi zaidi ya 5,000 hapa chuoni. “Hivyo kiwanda hicho licha ya kwamba kinatumika kwenye uzalishaji bali ni sehemu ya mafunzo kwa wanafunzi wao ambapo hata wataalamu wanaojua teknolojia hiyo watawaajiri baadaye,” alisema Profesa Chacha.
Amesema mita hizo zinatengenezwa na Watanzania kwa maana ya wataalamu wa ndani ambao pia wametengeneza mfumo mzima wa hizo mita na hata matengenezo wataalamu wa ndani ndio watakuwa wanafanya siku zote. “Kupitia hizi mita tutaweza kuharakisha maendeleo ya Watanzania kwani wanaotengeneza ni Watanzania na vijana watapata ajira kupitia uzalishaji huo kwani mchakato huo umekuwa ni jumuishi na utasukuma maendeleo ya Watanzania,” alisema Profesa Chacha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa, Wolta Kirita alisema uwekaji wa mita ni sehemu ya uwekezaji ambapo mita hizo zitafungwa kwa gharama za Ruwasa na kwa zile gharama ambazo wananchi wamechangia katika ununuzi wa maji.



