DC Ilala amaliza mgomo wa wafanyakazi wa kiwanda

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amemaliza mgomo wa wafanyakazi zaidi ya 1,500 wa Kiwanda cha Namera kilichopo Gongolamboto Dar es Salaam ulioanza Januari 16, mwaka huu. Mgomo huo ulitokana na madai ya mishahara ambapo kima cha chini kwa sekta binafsi kimewekwa kwa mujibu wa Tangazo na Amri ya Serikali Namba 605A ya Oktoba 13, 2025, inayotoa ongezeko la wastani wa asilimia 33.4.
Kutokana na ongezeko hilo, mshahara wa chini umeongezeka kutoka Sh 275,060 mwaka 2022 hadi Sh 358,222 mwaka 2025. Mpogolo amesisiriza kuwa Amri ya Serikali ni lazima itekelezwe na kwamba hakuna kampuni, taasisi au mwajiri yeyote anayekubalika kushuka chini ya viwango vilivyowekwa kisheria.
Mpogolo ametoa maelekezo muhimu kwa uongozi wa kiwanda na wafanyakazi, ikiwemo kuhakikisha malipo ya mishahara yanatolewa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 605A la mwaka 2025, huku akisisitiza kuwa hakuna mfanyakazi atakayefukuzwa kutokana na kushiriki mgomo ili kuimarisha mahusiano bora kati ya mwajiri na waajiriwa.
Aidha, alikitaka kiwanda kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi (TUICO) na Ofisa Kazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kufanyika uchaguzi wa viongozi wa wafanyakazi watakao kuwa kiungo kati ya wafanyakazi na uongozi, pamoja na kupitia mikataba ya ajira kuhakikisha inakidhi sheria na kanuni zinazohitajika. Mpogolo pia alihimiza mahusiano mazuri na kulinda kiwanda kutokana na mchango wake katika uchumi wa taifa na nafasi zake muhimu za ajira kwa wananchi.
Kwa upande wao wafanyakazi wa kiwanda hicho wameeleza kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Mkuu wa Wilaya, wakisema zimeleta matumaini mapya na kurejesha amani kazini na kuahidi kurejea kazini mara moja na kuendelea kutekeleza majukumu yao kama kawaida.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Yustino Mgonja amepongeza juhudi za Mpogolo kushughulikia mgogoro huo kwa haraka na kwa busara. Mgonja amesema hali ya usalama katika eneo la kiwanda ni shwari na amewahakikishia wafanyakazi kuwa wapo salama.
Amesema kuwa kiwanda hicho ni muhimu kwani kinatoa ajira, hivyo migogoro inaweza kuharibu upatikanaji wa ajira hizo na ukuaji wa uchumi. Kwa upande wake, mmiliki wa kiwanda hicho, Hamza Pardesi amesema yupo tayari kutekeleza makubaliano yote yaliyofikiwa kati ya uongozi wa kiwanda na serikali, huku akiahidi kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha ushirikiano kati ya waajiri na wafanyakazi kwa maslahi ya pamoja.
Kufuatia kumalizika kwa mgomo huo, shughuli za uzalishaji katika kiwanda hicho zinatarajiwa kurejea kama kawaida, wakati wafanyakazi wakirejea kazini wakiwa na ari mpya ya kufanya kazi. SOMA: NEMC yachukua hatua kiwanda bubu Kinondoni



