SUA yazalisha watalamu kilimo biashara

MOROGORO: CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia mtaala mpya wa masomo ya Shamba Darasa la Klimo Biashara (FFBS), kimetoa wataalamu wa kwanza nchini watakaokuwa na ubobezi ili kulisaidia taifa katika juhudi za kuleta mapinduzi endelevu yenye tija kwenye sekta ya kilimo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Rasel Madaha amesema hayo wakati wa maonesho ya mazao kupitia mashamba darasa ya kilimo biashara ya vikundi vitatu vya wakulima katika Manispaa ya Morogoro vilivyosimamiwa wataalamu hao.

Profesa Madaha amesema ,SUA imetoa kwa mara kwanza wataalamu wapatao 29 baada ya kuanzishwa mtaala mpya ulionzishwa mwaka uliopita unaofundisha shamba darasa la Kilimo Biashara ulianza kutumika mwaka jana kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza , shahada ya Uzamili na shahada ya Uzamivu.
“Tumetoa kwa mara kwanza wataalamu waandamizi , wabobezi hapa Tanzania na si Tanzania tu hata duniani hawapo, baada ya SUA kuwa ya kwanza kuingiza mtaala wa elimu ya shamba darasa la kibiashara kuwa somo kamaili na kuanza na Uzamili,” amesema Profesa Madaha.

Profesa Madaha amesema wataalamu hao wamepatikana kipindi muhimu ambacho Taifa kupitia Mwongozo ambao umeboresha mifumo ya shamba darasa na sasa yawe ni shamba darasa la kilimo kibiashara.
“Mwongozo huo unatutaka tuanzishe shamba darasa la kilimo cha kibiashara ,na ili kufikia malengo haya, SUA kupitia mtaala mpya tumezalisha wataalamu hawa wa kwanza kabisa hapa nchini ili waende kusaidia katika juhudi za kuleta mapinduzi ya sekta ya kilimo kwa wakulima,” amesema Profesa Madaha.
Profesa Madaha amesema wahitimu hao amba oni wafanyakazi serikalini katika sekta ya kilimo watatumia elimu na ubunifu wao kwenda kubadilisha kilimo kiwe cha kibiashara zaidi wakizingatia utafiti wa soko kwanza ili kuleta mapundizi yenye tija kwa wakulima.

Naye Mwanafunzi wa shahada ya Uzamili (MSC), Kija Kayenze amesema kuwa wakulima wengi wanakosa elimu sahihi ya namna ya kuongeza thamani ya mazao wanayoyazalisha na kuwasababishia wapate hasara pindi soko linapokosekana .
Kayenze ambaye ni Ofisa Kilimo Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu amewashauri wataalamu wa sekta ya kilimo na taasisi za kilimo kushirikiana nguvu kubwa ya kuwaopatia elimu wakulima ili waweze kuongeza thamani mazao yao na mamkala za serikali za mitaa zitenge bajeti kwa ajili ya wataalamu wa kilimo ili kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la Care International Tanzania , Christina John amesema Shirika hilo ni waanzilishi wa mbinu ya shamba darala la kilimo biashara nchini.

Christina amesema kutokana na uzoefu huo lilitoa ushauri mbinu hizo ziingiwe kwenye mitaala ya Vyuo Vikuu ambapo SUA ilipokea nakuhuisha mtaala wa shamba darasa la kibiashara na kulifanya liwe somo kamili kwa shahada ya kwanza, Uzamili na Uzamivu ili kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.



