ATCL inavyofungua uchumi Pemba

PEMBA ni moja ya visiwa vya Zanzibar vilivyo katika Ukanda wa Bahari ya Hindi.

Pemba ina historia ya utajiri wa maliasili na fursa nyingi za kiuchumi. Kisiwa hicho ni maarufu kwa zao la karafuu. Wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali nchini wamekuwa wakisafiri kwenda Pemba kupeleka na kuchukua bidhaa mbalimbali.

Moja ya mahangaiko ya wafanyabiashara ni usafiri wa uhakika kuwatoa na kuwafikisha kwenye kisiwa hicho kwa wakati. Serikali kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) imesikia kilio na kuanzisha safari za ndege kupitia ndege aina ya Bombardier Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 70.

Kwa mujibu wa ATCL, kwa kuanzia ndege hiyo itafanya safari za kutoka Dar es Salaam – Pemba kupitia Unguja mara tatu kwa wiki yaani Jumanne, Ijumaa na Jumapili. Hakuna shaka kuwa safari hizo zitakuwa kichocheo cha kuimarisha uchumi wa Kisiwani Pemba kwa kuongeza watalii, kuimarisha biashara na kupanua masoko ya bidhaa za ndani na nje ya nchi.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukitamani safari za Pemba kwa ndege kubwa kama hivi, imekuwa faraja kwa wafanyabiashara wa visiwa hivi. Naamini sasa biashara zetu zitapanuka na hii itasaidia kukuza uchumi wetu sisi na wa nchi yetu kwa ujumla,” anasema mfanyabishaara Ahmed Salum Ali aliyesafiri kwa ndege hiyo siku ya uzinduzi safari hiyo Agosti 20, mwaka huu.

SOMA: ATCL mguu sawa kuiunganisha Afrika

“Kwa kweli kupata usafiri huu sisi wakazi wa Pemba tumefarijika sana. Inakuwa rahisi kwenda Unguja na kuunganisha Dar es Salaam kwa shughuli mbalimbali iwe za kikazi ama kifamilia,” anasema mkazi wa Chakechake Pemba, Hafsa Ali Mahmoud.

“Mimi kama mwananchi wa Kisiwa cha Pemba nimefurahia sana kuja kwa usafiri huu kwa sababu ni fursa ambayo sasa inaendelea kuja katika visiwa vyetu hivi kwa lengo la kujenga na kuimarisha usafiri wa angani.”

“Naipongeza serikali kwa jambo jema na zuri walilotuletea katika kisiwa hiki na Zanzibar yetu kwa ujumla kwa sababu kuna mambo mengi ya utalii na biashara yanaweza kutokea katika kisiwa chetu kupitia usafiri huu,” anasema mkazi mwingine wa Pemba, Mohamed Abdi Said.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chakechake, Mgeni Khatib Yahya anasema anawashukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Hussein Mwinyi kwa mambo mazuri wanayoendelea kuyafanya.

“Tumeona namna Pemba inavyoendelea kuunganishwa na sehemu nyingine kwa kutumia usafiri huu wa ndege… Niseme tu kwamba usafiri huu utarahisisha mambo mengi ikiwemo kukua kwa uchumi wa taifa letu na uchumi wa mtu mmojammoja.”

“Tumeona ile azma ya Dk Mwinyi kuifungua Pemba inavyofanikiwa kwani sasa wageni wanazidi kuongezeka… usafiri huu kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni chachu ya maendeleo,” anasema. Mtendaji Mkuu wa ATCL, Peter Ulanga anasema jitihada za Serikali kwa usafiri wa anga zimekuwa na mafanikio makubwa.

Anasema uthibitisho wa hilo ni uzinduzi wa safari za Mtwara na Iringa uliofanyika Machi mwaka huu na pia, usafiri wa Kinshasa katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). “Safari hizi zimepokelewa vizuri sana sokoni na hii ni jitihada za muda mrefu za serikali na sasa zimezaa matunda,” anasema.

Anaongeza: “Takwimu zinaonesha zaidi ya abiria 320 hutumia ndege za ATCL katika safari za Iringa na wastani wa abiria zaidi ya 370 upande wa Mtwara na 500 kutoka Kinshasa kila wiki.” “Kwa kweli tunajivunia uwekezaji huu, kwa sasa ATCL tuna ndege mpya 15 na pia tuna ndege moja ya mizigo, kati ya hizo ndege saba zimenunuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia.”

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa anasema kupitia safari hizo Pemba sasa inaunganishwa moja kwa moja kwa mitandao ya safari za ndege nchini hususani visiwa vya Unguja na miji mikubwa ya Tanzania bara ikiwemo ya Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma na hapo uchumi wa Pemba utafunguka zaidi.

“Safari hizi pia zitaiunganisha Pemba na mitandao ya safari za kimataifa kama Dubai, Johannesburg (Afrika Kusini), Harare (Zimbabwe), Lusaka (Zambia), Mumbai (India), Guangzhou (China) na hivi karibuni Lagos nchini Nigeria,” anasema. Kwa mujibu wa Mbarawa, uamuzi wa kuanzisha safari hizo kupitia Unguja una faida nyingi zikiwemo za kiuchumi na kijamii.

“Kibiashara unafungua fursa kwa wafanyabiashara wa Pemba na Unguja kushiriki zaidi, kubadilishana bidhaa na kuunganisha masoko yao kwa ufanisi na kiutalii. Watalii wanaowasili Unguja sasa wana nafasi rahisi ya kuendelea na safari hadi Pemba bila usumbufu wa kupanga usafiri wa ziada na hivyo kuongeza idadi ya watalii wanaoingia katika visiwa vya Pemba,” anasema.

Anataja faida nyingine ni za kiulinzi na kiusalama kwani Kituo cha Unguja kinarahisisha usimamizi wa usalama wa abiria na mizigo kulingana na viwango vya kimataifa. Profesa Mbarawa anasema, “Na kijamii safari hizi zinaboresha mawasiliano na uhusiano wa kifamilia kati ya wananchi wa Pemba, Unguja na Tanzania bara.”

“Kama mnavyofahamu, sekta ya usafiri na usafirishaji ndiyo uti wa mgongo katika mnyororo wa ukuaji na uimarishaji wa uchumi, hivyo usafiri wa anga ni injini ya ukuaji wa uchumi wa taifa letu,” anasema.

Anaongeza: “Ndiyo maana Serikali zetu zimewekeza kwa kiwango kikubwa katika ununuzi wa ndege, uboreshaji wa viwanja vya ndege pamoja na uimarishaji wa huduma za kampuni yetu ya ndege. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa, kuimarisha muungano wetu na kuhakikisha uchumi wa bluu unaleta matunda kwa wananchi wote.”

Katika kuhakikisha huduma za usafiri huo zinakuwa nzuri na endelevu, Mbarawa anatoa maelekezo matano kwa uongozi wa ATCL ikiwemo kuhakikisha ratiba za safari za Dar es Salaam-Pemba kupitia Unguja zinafuatwa kwa ukamilifu huku ubora wa huduma ukidumishwa na kuimarishwa ili kuwaepushia abiria usumbufu.

“Kuzingatia viwango vya huduma na usalama wa kimataifa, huduma kwa wateja, usalama wa abiria na ubora wa ndege viwe ajenda ya kila siku…Aidha, nawaagiza kukuza masoko ya safari hizi, tekelezeni kampeni mahususi za masoko ndani na nje ya nchi ili kuongeza idadi ya abiria na watalii wanaoelekea Pemba,” anasema.

Agizo lingine ni kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) pamoja na wadau wa sekta ya utalii.

“Hakikisheni safari hizi zinachangia moja kwa moja kwenye uchumi wa visiwa na ustawi wa wananchi na pia,
msisahau kufanya tathmini endelevu ya mara kwa mara ili kutatua changamoto mapema, kuongeza ufanisi wa biashara pamoja na kuhakikisha safari zinabaki na faida,” anasema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button