Athari za El-Nino kugharimu bil 986/-

DODOMA: SERIKALI imesema matengenezo ya miundombinu iliyoathirika na mvua za El – Nino yanahitaji Sh bilioni 986.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema bungeni Dodoma jana na akaeleza kuwa kiasi hicho kilifahamika wakati wa tathmini iliyofanyika Aprili mwaka huu.

Bashungwa amesema hayo wakati akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25.

SOMA: Kinana ataka misaada zaidi waathirika Rufiji

Amesema mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha kwa takribani miezi tisa mfululizo kuanzia Septemba mwaka jana zimesababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja nchi nzima.

Amesema hadi Mei mwaka huu Hazina imetoa Sh bilioni 72 kwa ajili ya kazi za matengenezo ya dharura.

“Serikali inasubiri taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu kumalizika kwa msimu wa mvua ili itoe fedha zaidi na kutangaza zabuni za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya maeneo yote yaliyoathiriwa,” amesema Bashungwa.

Kimbunga Hidaya Bashungwa alisema kimbunga cha kitropiki chenye upepo wa kilometa 119 kwa saa kilichojulikana kwa jina la Hidaya, kimesababisha uharibifu wa miundombinu katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Kisiwa cha Mafia.

Amesema mvua kubwa zilizoambatana na kimbunga hicho zilisababisha kukatika kwa mawasiliano baina ya mikoa ya Pwani na Lindi eneo la Mikereng’ende, Songas, Somanga na Matandu – Nangurukuru.

“Kwa ujumla, uharibifu uliotokea katika barabara ya Mtwara – Lindi – Dar es Salaam ni mkubwa na hivyo barabara yote inatakiwa kujengwa upya,” amesema Bashungwa.

Ametaja maeneo mengine yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa ni katika barabara ya Nangurukuru – Liwale (daraja la Miguruwe, eneo la Zinga na eneo la Mlowoka); Kiranjeranje – Namichiga (daraja la mto Mbwemkuru na daraja la Kigombo) pamoja na Tingi – Kipatimu (eneo la mto Liomanga na eneo la mto Chumo).

“Tayari manunuzi kwa ajili ya ukarabati kwa kiwango cha lami wa kipande cha barabara ya Mtwara – Mingoyo yapo katika hatua za mwisho,” ameeleza Bashungwa.

Amesema tathmini ya gharama za kurudisha mawasiliano ya barabara yaliyoathirika iliyofanyika ilionesha mahitaji halisi kwa ajili ya matengenezo ya barabara hizo ni Sh bilioni 84.135.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za dharura ili kurejesha miundombinu iliyoathirika,” amesema Bashungwa.

Habari Zifananazo

Back to top button