WATU watatu wamefariki dunia katika matukio tofauti mkoani Mtwara, akiwemo mmoja aliyeuliwa kwa tuhuma za kula mayai ya biashara na baadaye kukataa kulipa.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani Mtwara leo Oktoba 25, 2022, imesema Juma Chimbende (34), alichomwa eneo la kifuani na kitu chenye ncha kali na Himid Mikidadi (23), akidaiwa kukataa kulipa fedha za mayai aliyokula.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, Kaimu Kamanda wa Polisi, ACP Nicodemus Katembo, amesema tukio hilo lilitokea Oktoba 23, mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi katika eneo la majengo manispaa ya Mtwara Mikindani.
Ameeleza kuwa katika uchunguzi uliofanywa na madaktari umebaini sababu ya kifo ni kuvuja damu nyingi katika jeraha kubwa alilolipata kifuani na kueleza kuwa idadi ya mayai aliyokula haijajulikana.
Amesema katika tukio lingine lilitokea Oktoba 21, mwaka huu, majira ya saa 12 jioni katika Kijiji cha Mbawala, Wilaya ya Mtwara, ambapo Waziri Mnyelema alifariki baada ya kupigwa mawe na magongo ya miti kwa tuhuma za kuvunja nyumba na kuiba.
Tukio lingine lilitokea Oktoba 22, majira ya saa tano asubuhi katika Kijiji cha Miwindi kata ya Mkunya, Wilaya ya Mtwara ambapo Mohamed Hamis (17), aliuawa kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali maeneo mbalimbali ya mwili wake na watu wasiofahamika kwa tuhuma za wizi.