Awamu ya pili, Madaktari bingwa wawasili Katavi

KATAVI: Awamu ya pili ya timu ya Madaktari bingwa 17 kutoka New York nchini Marekani wamewasili leo mkoani Katavi kwa ajili ya kambi maalum ya kutoa huduma ya upasuaji wa kibingwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika iliyopo mkoani Katavi.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea madaktari hao waliowasili katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda, Mganga Mkuu wa wilay ya hiyo Dk Alex Mrema amesema walitegemea kupokea madaktari bingwa 20 lakini watatu wamepata changamoto hivyo kushindwa kufika.

Amesema timu hiyo inayotarajiwa kuwepo kwa siku saba itajikita katika sehemu kuu nne ambazo ni magonjwa ya kichwa na shingo (Head and neck surgery), Goita, upasuaji wote uliopo eneo la tumbo pamoja na upasuaji eneo la mataya pamoja na kurudisha sura.

“Tutatoa huduma ya upasuaji kwa sababu ‘tumeshascreen’ mpaka sasa hivi tuna wagonjwa 140 kwa hiyo tunategemea kadri tutakavyoweza kufanya kwa wingi tuwafikie walau wagonjwa 100” amesema

Amesema madaktari wa awamu ya kwanza walifanya upasuaji kwa wagonjwa 69 kati yao wagonjwa 63 walifanyiwa upasuaji mkubwa.

Isome pia https://habarileo.co.tz/madaktari-bingwa18-wawasili-tanganyika/

Kwa upande wake Prof. Medhat Allam mmoja wa madaktari hao ambaye ni Mkurugenzi wa shirika la Operation International kwa niaba ya wenzake amesema wamefurahi kuja Tanzania hivyo wanatarajia kufanya upasuaji wa wagonjwa wengi kwa kadri ya uwezo wao.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Katavi wamesema ujio wa madaktari hao utawaondolea changamoto ya upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa kuwa wagonjwa wanalazimika kupata rufaa kwenda Mbeya, Bugando, Benjamin Mkapa na Muhimbili kufuata huduma hizo jambo ambalo ni gharama kubwa.

“Wengine wanafariki kwa kushindwa kumudu gharama wanapopewa rufaa,hivyo tunashukuru ujio wao kwani ndugu zetu wagonjwa watapona bila kusafiri”amesema Hamida Jumbe

Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo wa Shirika la Norbert & Friends Missions/Operation International wameleta wataalam hao na huduma hizo zitaendelea bila malipo hadi Mei 10, 2024.

Habari Zifananazo

Back to top button