Aweso ataka mikoa ‘kuwatumbua’ wakandarasi miradi ya maji

WAZIRI wa maji Jumaa Aweso amewataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nchini kusimamia kwa karibu miradi ya maji na kuwakemea na kuchukua hatua kwa wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza miradi kwa wakati.
Waziri Aweso ametoa maagizo hayo alipofanya ziara kutembelea na kukagua mradi wa maji wa Kasulu mkoani Kigoma wenye thamani ya sh Bilioni 35 ambao ni moja ya miradi inayotekelezwa katika miji 28 nchini.

Amesema serikali imeweka dhamira ya dhati kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa kila Mtanzania na kutafuta fedha ambazo tayari zimeelekezwa kwa wakandarasi hivyo hakuna sababu ya miradi hiyo kushindwa kutekeleza kwa wakati.
Kutokana na hilo amewataka wakuu wa mikoa kuwachukulia hatua wakandarasi wote wanaoshindwa kutekeleza miradi kwa wakati na kwamba wizara ya maji itatoa baraka kwa hatua zitakazochukuliwa.

Awali akitoa maelezo ya mradi kwa Waziri wa Maji, Mkurugenzi Mtendaji wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kasulu, Mhandisi Hussein Nyemba amesema mradi huo utakapokamilika utahudumia watu 187,343 kutoka kata 13 za mji wa Kasulu.
Nyemba amesema kwa sasa mradi umefikia asilimia 49 ya utekelezaji wake malengo yakiwa ni kuhakikisha unakamilika mwezi Oktoba mwaka huu ambapo kukamilika kwake kutawezesha lita za maji milioni 15 kuzalishwa na maji kupatikana kwa asilimia 100 kutoka asilimia 71 za sasa.



