Tunduru yapokea mradi wa oksijeni wa bil 1.5/-
HOSPITALI ya Wilaya ya Tunduru imekabidhiwa rasmi mradi wa uzalishaji na usambazaji wa hewa tiba ya oksijeni, unaogharimu sh bilioni 1.5 na ambao unatarajiwa kuongeza uwezo wa hospitali hiyo katika kuhudumia wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura na uangalizi maalum.
Makabidhiano ya mradi huo yamefanyika katika eneo la hospitali hiyo yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa sekta ya afya pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Afya.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru, Renatus Mathias ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuipatia hospitali hiyo mradi muhimu unaokwenda kupunguza changamoto ya upatikanaji wa hewa tiba, hususan wakati wa ongezeko la wagonjwa wanaohitaji msaada wa kupumua.
SOMA: Tunduru watakiwa kupanda miti maeneo yao
Amesema mradi huo utaongeza ufanisi katika kutoa huduma za dharura, wodi za wazazi, wagonjwa mahututi (ICU), pamoja na kitengo cha upasuaji, hivyo kuboresha kwa kiwango kikubwa huduma za afya kwa wakazi wa wilaya ya Tunduru na maeneo jirani.

Mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuongeza miundombinu ya huduma za afya nchini, hususan katika wilaya zinazohitaji maboresho ya haraka ya vifaa tiba na uwezo wa kuhudumia wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum.



