Aweso ataka utafiti upatikanaji maji Dodoma

DODOMA: WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewata wataalamu kufanya utafiti wa kina wa upatikanaji wa maji jijini Dodoma ili kuruhusu uchimbaji wa visima virefu kwa haraka katika mkoa huo kutatua tatizo la upungufu wa maji linalotokana na ongezeko la watu katika jiji hilo.

Aweso amesema hayo Oktoba 31,2024 akiwa katika ziara yake kwenye maeneo ya Miganga-Mkonze na Nkuhungu kuangalia hali ya upatikanaji maji jijini Dodoma.

“Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametupatia vifaa vya kisasa vya utafiti wa kina wa upatikanaji wa maji,nataka vianze kazi hiyo hapa Jijini Dodoma ili tuendelee na uchimbaji wa visima virefu kutatua adha ya upatikanaji wa maji iliyosababishwa na ongezeko kubwa la watu jijini Dodoma,” amesema Aweso.

Advertisement

Ameongeza kuwa wakati wakiendelea kusubiri mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria na mradi wa bwawa la Farkwa aliwataka watendaji wa maji waendelee kuchimba visima maeneo tofauti ili kuounguza adha ya maji ndani ya mkoa huo.

Aidha, amewasisitiza watumishi wa mamlaka kuhakikisha wananchi hawabambikiziwi bill za maji ili kuondokana na changamoto kubwa iliyolalamikiwa ya kubambikiwa bill za maji na kuwa wamejiandaa kuja na mfumo wa kulipa kadiri utakavyotumia.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amemshukuru Aweso kwa jitahada kubwa za utatuzi wa kero ya maji Dodoma na kuomba rasmi utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa maji wa Nzuguni A ambao utasaidia upatikanaji wa maji katika maeneo ya Ihumwa, Nzuguni,Ilazo, Mlimwa C, Kisasa, Mailimbili, Area C,Area D na Chamwino.

Amesema kwa kufanya hivyo maji yaliyokuwa yakielekezwa maeneo hayo yabadilishwe muelekeo kuwahudumia wananchi ambao awali mgawo wao wa maji ulikuwa mkubwa.

Akitia taarifa yake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma(DUWASA) , Mhandisi Aron Joseph amesema mahitaji ya maji jijini Dodoma kwa siku ni lita milioni 147 na huku uzalishaji wa maji ni lita milioni 79 na hivyo kuwa na upungufu wa lita milioni 68 kwa usiku hali inayopelekea mgao mkubwa wa maji.