Aweso azungumzia upungufu wa maji Mwanza

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewatoa hofu wakazi wa Jiji la Mwanza kuhusu upungufu wa maji katika kipindi hiki na kueleza kuwa serikali inatambua na jitihada za kuhakikisha adha hiyo inamalizika.

Aweso amesema hayo wakati wa ziara ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango katika Manispaa ya Ilemela, Mwanza.

“Naomba niwaambie ndugu zangu wa Ilemela baada ya dhiki sio dhiki baada ya dhiki ni faraja na faraja yenu ni Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango,” Waziri Aweso amebainisha Serikali inatambua upungufu wa huduma ya maji ihususan maeneo ya Buswelu na Ilemela na ufumbuzi umepatikana.

Amesema mahitaji ya maji katika Jiji la Mwanza ni lita milioni 160 wakati mitambo ya Capripoint uwezo wake ni kuzalisha lita milioni 90 maana yake ni kwamba kuna ongezeko la mahitaji ya maji ikilinganishwa na uzalishaji uliopo sasa.

Hata hivyo, Waziri Aweso amebainisha hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali ni pamoja na ujenzi wa dakio kubwa la maji eneo la Butimba ambalo kwa awamu ya kwanza litazalisha lita milioni 48 za maji kwa siku.

“Baada ya kuona upungufu huu wa maji, ukienda eneo la Butimba tuna mradi wa maji wa zaidi ya shilingi bilioni 69 mradio huu uliukagua na ulitupa maelekezo baada ya kutuwekea jiwe la msingi,” amefafanua Waziri Aweso.

Amesema mradi huo wa Butimba upo katika hatua nzuri na tayari ujenzi wa matenki na mitambo ya kuchuja maji imekamilika na kwamba changamoto ilikuwa pampu ambazo ziliagizwa nje ya nchi ambazo zimefika na hatua ya usimikaji wake inaanza hivi karibuni ili Mwezi Juni 2023 mradi uwe umeanza kutoa maji.

Baada ya kubainisha hali halisi ya upatikanaji wa huduma ya maji Jijini Mwanza na hatua zilizochukuliwa na Serikali, Waziri Aweso ameielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) yenye dhamana ya kuwafikishia maji wananchi wa Jiji la Mwanza kuhakikisha wakati huu wa upungufu wa maji wahakikishe wanakuwa na migao ya maji yenye tija.

Habari Zifananazo

Back to top button