Azam FC haiwahofii Pyramids

TIMU ya Azam FC imesema haiwahofii Pyramids FC ya Misri itakayokutana nayo mzunguko wa kwanza wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam FC itakutana na Horseed ya Somalia katika hatua za awali na ikipita itakutana na Pyramids mzunguko wa kwanza wa michuano hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema anajua Pyramids ni bora Afrika, lakini hawaiogopi, wanajipanga kupambana kufika mbali kwenye michuano hiyo.

“Tukipita hatua za awali tunakutana na vigogo hao wa Misri, ni moja ya timu nzuri, tunajipanga kuhakikisha tunashindana nao kufikia malengo yetu tuliyokusudia,” alisema.

Popat alisema hawadharau wapinzani wao wajao timu hiyo ya Somalia kwani mpira wa Afrika unabadilika na pengine wanaweza kukutana na ushindani mkali.

“Tunawaheshimu Horseed huku tukijipanga  kufanya vizuri ili tukutane na Pyramids kuendelea kudhihirisha ubora wetu,” alisema.

Mechi za awali za michuano hiyo zitachezwa kati ya Septemba 10-12 kwa mkondo wa kwanza na zile za marudiano zitapigwa wiki moja baadaye.

Wanalambalamba hao wa Chamazi kwa sasa wanaendelea na kambi ya siku 10 Azam Complex, kisha wiki ijayo watakwenda kukaa siku nyingine 10 za maandalizi ya kimataifa nchini Zambia.

Habari Zifananazo

Back to top button