Azid Ki, Chama wamkosha Miloud

DAR ES SALAAM – KOCHA Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi amesema ameridhishwa na kiwango cha Stephane Aziz Ki pamoja na Clatous Chama walichoonesha katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Stand United uliochezwa KMC Complex Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, mabingwa hao watetezi Yanga walitinga nusu fainali na sasa watakabiliana na JKT Tanzania katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga Mei 16, mwaka huu.

Akizungumza baada ya mchezo huo juzi, Miloud alisema amefurahia Yanga kutinga nusu fainali na zaidi ameridhishwa namna nyota hao walivyocheza, akieleza kuwa wamejibu maswali mengi ya mashabiki.

Alisema, Aziz Ki ametoka kwenye majeraha lakini alijituma kwa kiwango cha juu kuanzia mazoezini na juzi aliwajibu wote waliokuwa na mashaka naye.

Kuhusu, Chama alisema hana shaka naye kwani anatambua ni mchezaji mkubwa na anapokuwa kwenye ubora wake kama juzi, hakuna namna timu pinzani wanaweza kumzuia.

Aliongeza kuwa aliwaeleza wachezaji wote kuwa anataka wamalize msimu huu wakiwa imara na hicho kilidhihirika kwa aliowapa nafasi alipofanya mabadiliko.

Naye Kocha Mkuu wa Stand United, Juma Masoud alisema mpango wao wa kuwadhibiti Yanga haukufanikiwa. Alisema walifanya makosa yaliyosabisha kufungwa mapema, hivyo kuwatoa mchezoni huku akidai uchanga wa wachezaji wake umewagharimu.

Wakati huo huo, nusu fainali ya Simba na Singida Black Stars itachezwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati Manyara, Mei 18, mwaka huu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button