Azimio la Tanzania kuwasha moto mpya korosho Afrika

TANZANIA imeibuka kuwa kinara wa kimataifa katika sekta ya korosho, ikiongoza mwito wa pamoja wa Afrika wa kusitisha mauzo ya korosho ghafi na kuwekeza kwenye uchakataji wa ndani.

Mwito huo wa kimkakati unaotarajiwa kuidhinishwa rasmi kama ‘Azimio la Tanzania’ utakuwa kitovu cha Mkutano wa Korosho Afrika 2025, unaotarajiwa kufanyika Mtwara kuanzia Novemba18 hadi 22, 2025.

Takwimu za Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) za mwaka 2024 zinaonesha ongezeko kubwa la uzalishaji katika misimu miwili mfululizo. Msimu wa kwanza ni wa mwaka 2023/2024 ilipozalisha zaidi ya tani 310,000 huku msimu mwingine wa 2024/2025 ikizalisha zaidi ya tani 528,000 kiwango ambacho ni cha juu zaidi katika historia ya taifa na Afrika kwa ujumla.

Kwa mujibu wa takwimu za vyanzo mbalimbali, zaidi ya kaya 700,000 ambazo ni takribani Watanzania milioni 2.5 zinategemea zao hilo kwa kipato cha moja kwa moja. Sekta ya korosho sasa inachangia zaidi ya Dola za Marekani milioni 400 kwa mwaka katika mapato ya fedha za kigeni.

SOMA: Maofisa ugani 500 waajiriwa uzalishaji korosho

Huu ni mchango muhimu wa pili baada ya tumbaku katika mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi. Vyanzo vinabainisha kuwa, ubora wa kipekee wa korosho zinazozalishwa Tanzania hasa katika mikoa ya Mtwara na Lindi ndio unaoipa Tanzania hadhi kubwa na ya kipekee duniani.

Ubora huu kwa mujibu wa vyanzo unatokana na ukweli kuwa, takribani asilimia 90 ya korosho ya Tanzania hulimwa kiasili bila matumizi ya mbolea za viwandani. Jambo hilo linaendana na matakwa ya wateja wa kimataifa wanaothamini bidhaa asilia na salama kiafya.

Afrika inazalisha zaidi ya asilimia 55 ya korosho ghafi duniani, lakini inachakata chini ya asilimia 15 ya mazao yake. Hali hii inasababisha hasara kubwa ya kimapato. Kilo moja ya korosho ghafi huuzwa kwa takribani kati ya Dola za Marekani 1.20 na 1.50.

Takwimu za Shirika la Chakula Duniani (FAO) za mwaka 2024, zinaonesha kuwa korosho iliyosindikwa hufikia bei ya hadi Dola za Marekani kati ya 10 na 12 katika masoko ya Ulaya, Asia na Amerika Kaskazini. Nchi kama Vietnam na India ambazo ni waingizaji wakuu wa korosho za Kiafrika ndizo wanufaika wakuu wa thamani ya uchakataji, wakipata faida mara nyingi zaidi ya wakulima na wachuuzi wa Afrika.

Ripoti za Benki ya Dunia zinaonesha kuwa, Bara la Afrika likiweza kuchakata hata nusu ya mazao yake, linaweza kupata zaidi ya Dola za Marekani bilioni 3 hadi 4 kila mwaka kama mapato ya ziada.

Soko la dunia la korosho linaendelea kukua kwa kasi, likitarajiwa kufikia thamani ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 15 ifikapo mwaka 2030. Hali hiyo inachochewa na ongezeko la ulaji wa vitafunwa vyenye protini nyingi na bidhaa mbadala za mazingira.

Azimio la Tanzania; mwito wa Afrika
Katika mkutano wa Mtwara, viongozi wa serikali, wakulima, wawekezaji na wadau wa kimataifa wanatarajiwa kujadili na kuidhinisha hatua mbalimbali za kimapinduzi. Hatua hizo ni pamoja na kusitisha mauzo ya korosho ghafi ifikapo mwaka 2027 na bara zima liweze kuzuia usafirishaji wa korosho ghafi ili kuchochea ujenzi wa viwanda vya ndani.

Nyingine ni suala la alama za kijiografia na hati miliki ili kulinda chapa na asili ya korosho kama korosho za Mtwara. Hii itaongeza thamani, itazuia uporaji wa maarifa na hata kudumisha ubora. Taarifa zinaitaja hatua ya tatu kuwa ni Sekretarieti ya Kimataifa ya Korosho kuanzishwa Mtwara kama kitovu cha utafiti, sera na ubunifu na kuufanya mji wa Mtwara kuwa ‘Davos ya Korosho.’

Kiuhalisia, Davos ni mji nchini Uswisi ambao ni maarufu kwa kuwa ni mwenyeji wa Mkutano wa Uchumi wa Dunia (World Economic Forum – WEF) unaofanyika kila mwaka ukikutanisha watu mashuhuri kutoka sekta za siasa, biashara, teknolojia na utetezi wa haki kujadili masuala mbalimbali yakiwamo ya uchumi wa kidunia.

Mengine ni Makumbusho na Kituo cha Utafiti wa Korosho ili kuhifadhi urithi wa korosho na kuendeleza teknolojia rafiki wa tabianchi na mbinu za kilimo endelevu pamoja na Wiki na Siku ya Korosho kuimarisha uhamasishaji, biashara, ubunifu na mshikamano wa bara zima.

Fursa za kiuchumi nakimazingira
Sekta ya uchakataji korosho inakisiwa kutoa mamilioni ya ajira za kijani, hususani kwa wanawake na vijana pamoja na kuchangia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 3 hadi 4 kwa mwaka ambayo ni angalau nusu ya korosho za Afrika zitazochakatwa barani.

Viwanda vya ndani vitapunguza utegemezi wa masoko korosho ghafi na kuongeza mapato ya kigeni, huku vikichochea ukuaji wa sekta za usafirishaji, vifungashio na teknolojia. Miti ya mikorosho hustahimili ukame, huongeza uhifadhi wa kaboni na kusaidia kurejesha ardhi iliyoharibika, hivyo kuwa muhimu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Wataalamu wa mazingira wanasema ongezeko la mashamba ya mikorosho linaendana moja kwa moja na mikakati ya Afrika ya kufikia malengo ya ‘net-zero’ yaani kiasi cha gesi chafuzi (kama vile kaboni daiyoksaidi) kinachozalishwa na binadamu kinalingana na kiasi kinachoondolewa au kufyonzwa kutoka angani kupitia miti, teknolojia za kunasa kaboni, au mabadiliko ya matumizi ya ardhi.

Chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania inalenga si tu kuongeza uzalishaji, bali pia kuifanya nchi kuwa kitovu cha uchakataji na biashara ya kimataifa ya korosho.

Serikali imeanzisha sera za kuhamasisha uwekezaji, kutoa mikopo kwa wakulima pamoja na kuboresha miundombinu ya bandari na barabara ili kupunguza gharama za usafirishaji. Kampuni binafsi na mashirika ya maendeleo nayo yanashirikiana kuanzisha viwanda.

Mwandishi ni Mwasisi wa Umoja Conservation Trust.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button