Baleke katikati ya Dube na Mzize Yanga

Baleke Baleke
Baleke

DAR ES SALAAM – KLABU ya Yanga imeachana na mshambuliaji wake Joseph Guede kutoka Ivory Coast na nafasi yake imechukuliwa na Jean Baleke.

Usajili wa mfumania nyavu huyo wa zamani wa Simba, TP Mazembe na Al Ittihad ya Libya unaenda kuongeza ushindani mkali kwenye kikosi cha Yanga kwenye msimu wa mwaka 2024/25.

Tayari klabu hiyo inaelezwa kupata saini ya mshambuliaji Prince Dube kutoka Azam na ambaye wadau na wachambuzi wa mpira wa miguu wanamchukulia kama ndiye atakayekwenda kuwa mshambuliaji kinara ndani ya Yanga.

Advertisement

Wakati wachambuzi na wadau hao wakiweka matumaini makubwa kwa Dube, Yanga wakanasa saini ya Baleke ambaye ni kama Dube ana uzoefu wa ligi na michuano ya kimataifa na ambaye bila shaka anaenda kuibua vita mpya ya namba katika eneo hilo.

Baleke ambaye aliachwa na Simba wakati wa dirisha dogo la usajili msimu wa mwaka 2023/24, aliifungia timu hiyo mabao manane na kutengeneza lingine moja, amepiga mashuti 19 na kati ya hayo 14 yalilenga lango na anatajwa kuongoza usahihi wa kupiga mashuti akiwa na asilimia 74 akifuatiwa na Joseph Guede mwenye asilimia 70, Dube asilimia 65 na Chama asilimia 63.

Alijiunga na Simba dirisha dogo msimu wa 2022/23 na kufunga mabao manane kwenye mechi tisa alizocheza, anaenda kushindana na Dube ambaye msimu huu kabla ya kujiengua kwenye kikosi cha Azam alikuwa amefunga mabao saba na kutengeneza mengine mawili.

SOMA: Chama awaaga rasmi Wanamsimbazi

Baleke pia atakabiliwa na ushindani mkali wa namba kutoka kwa mshambuliaji chipukizi wa timu hiyo Clement Mzize ambaye kwenye Ligi Kuu msimu wa 2023/24 amefunga mabao sita na kutengeneza mengine saba katika mechi 29 alizoichezea Yanga.

Dube, Mzize na Baleke kwa takwimu hizo ni wazi wanaenda kutengeneza ushindani mkali wa namba ambao utakuwa na faida kubwa kwenye kikosi cha Yanga msimu wa 2024/25