Bandari, reli zachochea Tanga ya Viwanda

TANGA ni miongoni mwa mikoa ya mwanzo kabisa nchini kuwa na viwanda vikubwa vya uzalishaji tangu miaka ya 1960.

Miongoni mwa viwanda hivyo ni Kiwanda cha Saruji cha Tanga, Amboni Sisal pamoja na kiwanda cha kutengeneza bidhaa za sabuni cha Fomu. Uwepo wa viwanda hivyo na vingine mkoani hapa umewezesha uzalishwaji wa ajira kwa Watanzania.

Serikali imekuja na mpango unaolenga kubadilisha Mkoa wa Tanga kuwa kitovu cha viwanda nchini kama ilivyokuwa hapo awali. Mpango huo ni sehemu ya utekelazaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 inayolenga kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa viwanda unategemea uzalishaji wa bidhaa zenye thamani ya juu.

Akiwa katika ziara mkoani Tanga Februari 2025, Rais Samia Suluhu Hassan anasema serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na wafanyabiashara ili Tanga Mkoa wa Tanga uwe mfano wa maendeleo ya viwanda nchini.

Uzalishaji katika kiwanda cha katani cha Amboni Plantations Ltd mkoani Tanga.

“Tanga ni lango kuu la uchumi wa Kaskazini, tuna dhamira ya kuufanya mkoa huu urejee kwenye hadhi yake kama kitovu cha viwanda na biashara,” anasema Rais Samia katika ziara hiyo.

Ili kuvutia wawekezaji serikali imewekeza katika uboreshaji wa miundombinu muhimu kama vile Bandari ya Tanga, ukarabati wa Reli ya Tanga hadi Arusha pamoja na miradi ya umeme na maji katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda.

Utekelezaji wa dhamira hiyo umeanza kudhihirika baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah kufanya ziara ya kikazi na kukagua baadhi ya viwanda ambavyo vimeanza kufufuliwa na  wawekezaji.

SOMA: Maboresho Bandari ya Tanga yalipa

Miongoni mwa viwanda hivyo ni Kiwanda cha Foma ambacho sasa kinazalisha bidhaa yake maarufu ya sabuni ya ‘foma’, kiwanda cha kuzalisha chuma sambamba na kiwanda cha kutengeneza bidhaa za mbao. Akiwa mkoani humo, anasema viwanda hivyo vinatarajiwa kuanza uzalishaji ifikapo Januari, 2026 baada ya kukamilika kwa ufungaji wa mitambo sambamba na majaribio ya uzalishaji wa bidhaa.

Anasema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia kuitaka wizara hiyo kukaa pamoja na wawekezaji hususani wenye viwanda na kujadili kwa pamoja changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi. “Kwa hapa Tanga, Rais ametaka tuangalia yale ambayo wenye viwanda waliiambia serikali lakini na sisi tuliwaelekeza na hivyo, ziara hii ni sehemu ya kujionea utekelezaji wa makubaliano hayo,” anasema katibu mkuu huyo.

Anasema anafurahishwa na namna wawekezaji wa viwanda hivyo walivyoonesha jitihada za kuanza kufufua viwanda vyao kwa uwepo wa mashine huku vingine vikiwa katika hatua za majaribio ya kuanza uzalishaji.

Akizungumzia kiwanda cha uchakataji wa bidhaa za misitu, magogo pamoja na uzalishaji wa bidhaa za mbao  anasema tayari serikali kupitia kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wametoa malighafi kwa ajili ya kiwanda kwa miaka mitano pindi kitakapoanza uzalishaji wake.

Anasema hatua hiyo inalenga kuhakikisha serikali inaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa viwanda kufanya shughuli zao bila vikwazo pamoja na kuhakikisha wananchi wetu wanapata fursa za ajira katika viwanda hivyo. Kuhusu viwanda vingine, Dk Abdallah anasema vipo katika hatua nzuri kwani kuna mashine mpya zimeshaletwa ingawa hazijafungwa. Anaahidi kuanza uzalishaji rasmi Januari, 2026.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa kutuwezesha kisera na kimiongozo ambayo inawezesha ufufuaji wa viwanda katika mkoa huu,” anasema. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batlida Buriani anasema takribani viwanda vitano vilivyokuwa vimefungwa vimeanza kufufuliwa na kuanza uzalishaji upya.

Anasema hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kuchochea maendeleo ya kiuchumi mkoani humo. Anasema tayari kuna kampuni mbili zilizojipanga kuanzisha viwanda vipya kikiwamo cha kuzalisha magari ya wagonjwa pamoja na kingine cha kuchakata tumbaku ambayo zao linalostawi katika mikoa ya Kaskazini Mashariki.

Aidha, anasema tayari viwanda vingine vitatu vipya wawekezaji wake wapo katika hatua za mwisho za majadiliano na serikali na kwamba majadiliano hayo yakikamilika, wataanza hatua za uwekezaji kwenye mkoa huo.

Anasema Mpango wa Tanga ya Viwanda umeongezwa chachu na uboreshwaji wa Bandari ya Tanga sambamba na reli miundombinu ambayo inayotoa uhakika wa usafirishaji wa malighafi na bidhaa haraka na kwa gharama nafuu.

Kwa mujibu wa Dk Burian, kupitia ufanisi wa Bandari ya Tanga, kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wawekezaji kuonesha nia ya kufanya uwekezaji hususani wa viwanda kwenye maeneo tofauti ya mkoa huu. Anasema tayari mkoa umezielekeza halmashauri zote kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya uwekezaji wa ndani na nje ya nchi yatakayokuwa na miundombinu yote muhimu ikiwemo umeme, maji na barabara.

“Huu ni wakati wa Tanga kusimama imara katika ajenda ya kitaifa ya uchumi wa viwanda kwani tunahitaji kuona viwanda vikizaliwa, vikikua na kuchangia ajira na mapato sambamba na maendeleo ya wananchi,” anasema Burian.

Anasisitiza serikali ya mkoa ipo tayari kushirikiana na wawekezaji wote kwa kuhakikisha kunakuwa na miundombinu muhimu na ya uhakika, sera rafiki na ufuatiliaji wa karibu ili kuondoa vikwazo katika ukuaji wa uchumi na viwanda mkoani Tanga.

Wawekezaji wa viwanda wanapongeza serikali kwa kuja na Mpango wa Tanga ya Viwanda wakisema utasaidia kuongeza fursa za ajira kwa wananchi huku pia ukiongeza tija kwa wawekezaji. Ofisa Rasilimali Watu wa kiwanda cha kuzalisha sabuni cha African Harmony Industries, Ahmed Mustafa anasema wanashukuru serikali kwa namna inavyosimamia makubalino yao katika mchakato wa ufufuaji wa viwanda.

“Serikali tumekuwa nao katika kila hatua za ufufuaji wa viwanda na wametusaidia kutatua changamoto kwa wakati,” anasema. Mustafa anaongeza: “Hiyo inaonesha dhamira waliyonayo kuhakikisha viwanda mkoani Tanga vinafufuka na kuanza kufanya kazi.”

Msimamizi wa Kiwanda cha Kuzalisha Bidhaa za Misitu, Hussein Abdallah anawataka wananchi wa Mkoa wa Tanga kujiandaa kutumia fursa za nyingi zijazo za ajira kwani kiwanda chao kitakuwa na uwezo wa ajira zaidi ya 1,000 katika hatua ya awali. Anasema ajira hizo zitakuwa zikiendelea kuongeza kadiri uzalishaji utakavyokuwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button