Benki, Serikali meza moja ufadhili elimu ya juu

DODOMA: Katika kuendelea kuunga mkono juhudi za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutekeleza mageuzi makubwa ya elimu nchini, timu ya Benki ya Exim ikiongozwa na Afisa Mkuu wa Fedha, Shani Kinswaga amekutana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda jijini Dodoma kwa lengo la kujadili namna taasisi hiyo inaweza kushirikiana na Serikali kutoa udhamini kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Kinswaga aliambatana na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na wa kati Andrew Lyimo na Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano Stanley Kafu.
Mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Benki ya Exim katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya elimu, zikiwemo fursa za ufadhili wa wanafunzi wa elimu ya juu hususan wanaosomea sayansi ya data (Data Science), akili unde (Artificial Intelligence) na sayansi shirikishi.
Majadiliano hayo pia yaliangazia fursa mbalimbali, ikiwemo uwezekano wa kupata ufadhili kutoka benki hiyo, hususan kwa wanafunzi wa elimu ya juu wanaosomea Sayansi ya Takwimu (Data Science) na Akili Unde (Artificial Intelligence), pamoja na kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza ujuzi wa kisasa unaohitajika katika soko la ajira la sasa na la baadaye.
Pande zote mbili zilisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuiwezesha Tanzania kwenda sambamba na mabadiliko ya kidijitali duniani. Exim Bank ilieleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na serikali katika kulea vipaji vya vijana na kujenga uwezo wao kupitia ufadhili, mafunzo na programu mbalimbali za maendeleo.
Kwa upande wake, Waziri alieleza kuridhishwa na utayari wa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuboresha elimu nchini, akibainisha kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kufanikisha malengo ya mageuzi ya elimu yanayolenga kujenga nguvu kazi yenye ujuzi wa hali ya juu.
Mkutano huo umefungua milango ya ushirikiano mpana zaidi kati ya Wizara na Exim Bank, huku ukitarajiwa kuanzishwa kwa miradi na programu zitakazochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya elimu nchini.



